Na Sophia Kingimali
Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha watu wenye ualbino (TAS) wameutaka uongozi wa Klabu ya Simba Sports kuomba radhi kwa watu wenye ualbino na umma kwa ujumla kufuatia kitendo kilichofanywa siku ya kilele cha Klabu hiyo (SIMBA DAY) cha kumtumia mtu mwenye ualbino kutembea nusu utupu mbele ya maelfu ya watu.
Akisoma tamko hilo Agosti 9, 2023 Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa TAS Taifa Godson Mollel amesema kuwa, kwa miaka mingi kumekuwa na jitahada mbalimbali za kuwatetea na kuwapigania watu wenye ualibino kutokana na madhira yaliyokuwa yakiwakumbuka ikiwemo mauaji na hata kukatwa baadhi ya viungo vya miili yao kwa kile kilichodaiwa walikuwa wakisaidia kupatikana kwa utajiri kwa baadhi ya watu.
Amesema kwa mujibu wa Ibara ya 12 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inaeleza kuwa, kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
“Tukio hili linafuatia tukio lingine lililofanywa na timu hii mwaka jana kwenye siku hiyo hiyo ya Simba day ambapo kilitokea kitendo cha kutengeneza jeneza na msalaba na kumnasibu mtu mwenye ualbino kama msukule,” amesema Mollel
Aidha ametoa wito kwa watu wenye ualbino wa kutokukubali kutumiwa hususani katika mambo yanayotweza utu wao.
“Tunatoa wito kwa jamii ikiwemo watu wenye ualbino wenyewe kutochukulia vitendo vya aina hii kwa wepesi na badala yake kuvikemea vikali kwa maana watu wenye ualbino ni binadamu kama binadamu wengine wenye haki ya kutokudharirishwa na kuheshimiwa utu wao,” ameongeza Mollel
Kwa upande wake Mkurugenzi wa LHRC Dkt. Anna Henga amesema utani wa jadi uliopo kati ya timu ya Simba na Yanga hauhalalishi vitendo vya kutweza utu wa mtu.
“Tunaiomba serikali na TFF kusimamia, tunataka Simba iombe radhi na wasipofanya hivyo hatua zàidi za kisheria zitachukuliwa, ” amesema Henga
Aidha Henga ameongeza kuwa Taasisi zote zenye ushawishi katika jamii hususani timu kubwa za Mpira kuepukana na vitendo hivi badala yake kujikita katika kuhamasisha heshima kwa utu wa watu wenye ualibino nchini.
Ibara ya 8 ya Mkataba wa Kimataifa wa watu wenye ulemavu inasisitiza jamii kuelimishwa kuhusu masuala ya ulemavu na serikali kutilia mkazo zàidi kukomesha masuala ya ubaguzi, udhalilishaji, unyanyasaji, dhana potofu dhidi ya watu wenye ulemavu na vitendo vyote vinavyotweza utu wa watu wenye ulemavu ikiwemo watu wenye ualbino, vilevile Sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 inataka watu wote kuzingatia ulinzi wa watu wenye ulemavu na kukomesha unyanyasaji na udhalilishaji.