K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, MBEYA
WAFANYAKAZI
wameipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kuanzisha Mfuko wa Fidia kwa
Wafanyakazi (WCF) kwani ni msaada mkubwa kwa waajiri hususan linapokuja suala
la kusaidia wafanyakazi wanapoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.
Wakizungumza
kwenye kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Tanzania 2023 maarufu kama
Nanenane katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, wamesema wao kama
wafanyakazi ndio wanufaika wakuu wa Mfuko huo, baada ya waajiri wao kujisajili
WCF.
Dkt.
George Mufulu, Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro, amesema kabla ya
kuanzishwa kwa WCF waajiri walikuwa wanaingia gharama kubwa sana kuwahudumia
wafanyakazi wao pale wanapopatwa na majanga mbalimbali wawapo kazini.
“Mimi
binafsi nimekuwa nikifahamu huduma mbalimbali za WCF kwa kweli Serikali
inapaswa kupongezwa kwa uamuzi wake wa kuanzisha chombo hiki, kwa sababu huko
nyuma waajiri walikuwa wakiingia gharama kubwa sana kuwahudumia wafanyakazi wao
pale wanapokuwa wamepatwa na majanga mbalimbali wawapo kazini.” Alisema.
Naye
Mwalimu Mkuu Msaidizi Shule ya Sekondari Wenda iliyoko Mbalizi, Mbeya, Neema Ngailo amesema WCF imesimama kwa
niaba ya wafanyakazi na waajiri linapotokea suala la mfanyakazi kupatwa na
madhila kutokana na kazi.
“Ile
namna ya kunifanya nijione kama sijaachwa peke yangu ni jambo la faraja na
nitoe wito kwa waajiri ambao bado hawajajisajili au wanalega lega kujiunga na
WCF wafanye hima, ni Mfuko unaotoa hakikisho kwa mtumishi pindi anapokumbwa na
majanga awapo kazini.” Alisema.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, amesema Mfuko umejiandaa
kusajili wanachama wengi zaidi kutokana na jitihada za Serikali za kutengeneza
ajira kupitia kilimo.
“Tumeungana
na Serikali yetu ya awamu ya sita ambayo imekuwa ikipambania sana kutengeneza
ajira kwa ajili ya vijana na akina mama kupitia mipango mbalimbali ya kuwaandaa
vijana ili kushiriki katika kilimo biashara na pindi watakapoanza shughuli zao
na kuajiri, watastahili kuwa wanachama wa WCF.” Alisema.
Elimu ya fidia kwa wafanyakazi ikiendelea kutolewa kwenye banda la WCF Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli (kulia) akifurahia jambo na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba walipokutana kwenye banda la WCF.