Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA William Mwakilema amesema Maonesho ya Nanenane ni jukwaa sahihi la kutangaza vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji vinavyopatikana katika Hifadhi za Taifa Tanzania kutokana na watu wengi wa ndani na nje wanaokuja kupata elimu na kununua bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wakulima, wafugaji na wafanyabiasha kutoka ndani na nje ya nchi.
Ameyasema hayo katika banda la TANAPA leo tarehe 08.08.2023 alipoungana na watanzania wengine katika maadhimisho ya kilele cha maonesho ya wakulima almaarufu Nanenane yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Akiwa katika banda la TANAPA na baadaye banda la TFS Kamishna Mwakilema alisema, “Taasisi za Maliasili na Utalii zinafurahia uwepo wa maonesho haya ya wakulima kwa sababu ni sehemu sahihi ya kutangaza vivutio vya utalii, kuwatangazia wananchi mazao ya utalii, mazao ya misitu na nyuki, pia kutangaza fursa za uwekezaji unaochagizwa na wingi wa watu wanaohudhuria maonesho haya.”
Aidha, Kamishna Mwakilema aliongeza, “kilimo na mifugo ambayo maonesho haya yanawalenga zaidi, wanategemea maji ambayo vyanzo vyake vikuu vimehifadhiwa katika hifadhi za taifa, vile vile utalii huongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao ya kilimo na mifugo. Hili linajidhihirisha kwa watalii wanapokuja kutalii nchini wanatumia chakula kinachozalishwa na wakulima na wafugaji wetu.”
Wananchi wengi waliotembelea banda la TANAPA walitaka kujua gharama za viingilio, malazi na jinsi ya kufika katika maeneo yenye vivutio vya utalii na maeneo ya Malikale. Aidha, wataalamu wa Uhifadhi kutoka TANAPA waliwaelimisha wananchi hao na kuahidi kutembelea vivutio vya utalii vinavyopatikana upande huu wa Kusini ikihusisha Hifadhi za Taifa Ruaha, Kitulo, Katavi na maeneo ya malikale ya Isimila na Kalenga.