Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Naibu Gavana, Bw. Julian Banzi Raphael alipofika katika banda la BoT kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima – Nanenane yaliyofanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya. Kulia ni Meneja Mawasiliano BoT, Bi. Victoria Msina.
……………………..
Benki Kuu ya Tanzania imetawazwa Mshindi wa Kwanza Kitaifa katika Kundi la Taasisi za Udhibiti, Ubora na Viwango katika Maonesho ya Wakulima – Nanenane yaliyohitimishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 8 Agosti jijini Mbeya.
Aidha, Benki Kuu imeshiriki katika Maonesho ya Nananane Zanzibar na katika Kanda zaa Kati jijini Dodoma, Kaskazini jijini Arusha, Kusini huko Lindi na Kanda ya Ziwa jijini Mwanza. Katika kanda zote, BoT imeibuka Mshindi wa kwanza katika Kundi la Mamlaka za Udhibiti na Usimamizi.
Maonesho hayo ya kimataifa yaliyofanyika katika viwanja vya John Mwakangale yalifunguliwa rasmi tarehe 01 Agosti 2023 na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ambaye pia alitembelea banda la Benki Kuu na kujionea namna wataalamu wake wanavyotoa elimu kwa wananchi.
Banda la Benki Kuu lilikuwa mojawapo ya vivutio muhimu katika maonesho hayo, na lilipokea wageni wengine mashuhuri wakiwemo Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Waziri Mkuu Mstaafu, Bw. Mizengo Pinda, pamoja na Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge ya Bajet, na Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo. Naibu Gavana, Bw. Julian Banzi Raphael, aliongoza ujumbe wa Benki Kuu katika kushiriki maonesho hayo, na pia alikuwa mwenyeji wa wageni hao mashuhuri.
Benki Kuu ilichukua fursa ya maonesho hayo kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya kiuchumi na fedha. Elimu hiyo ilihusu utafiti na sera za uchumi, uwekezaji katika dhamana za serikali, usimamizi wa mifumo ya malipo ya taifa na sekta ya fedha.
Aidha, walijifunza kuhusu kazi za Bodi ya Bima ya Amana, mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania, utatuzi wa malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha, na utambuzi wa alama za usalama katika noti zetu.
Zaidi ya hayo, Benki Kuu ilipata maoni na ushauri muhimu kutoka kwa wadau na wananchi mbalimbali kuhusu jinsi ya kuwafikia na kuwahudumia vyema, huku ikiendelea kuboresha utendaji wake katika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi.
Ushindi huu wa Benki Kuu ya Tanzania katika Maonesho ya Nanenane kitaifa na kikanda ni uthibitisho wa juhudi zake za kuchangia katika maendeleo ya nchi kwa kutoa elimu na huduma bora kwa wananchi na wadau wa sekta ya fedha.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, akisalimiana na Naibu Gavana, Bw. Julian Banzi Raphael alipofika katika banda la BoT kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima – Nanenane yaliyofanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya. Katikati ni Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo wakipewa maelezo na Mchambuzi Mkuu wa Masuala ya Fedha kutoka Kurugenzi ya Masoko ya Fedha BoT, Bw. Ephraim Madembwe kuhusu uwekezaji katika dhamana za serikali walipotembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane jijini Mbeya. Wapili kutoka kulia ni Naibu Gavana, Bw. Julian Banzi Raphael.
Afisa Mkuu Mwandamizi wa Benki kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sarafu BoT, Bi. Crispina Nkya, akitoa elimu ya utambuzi wa alama za usalama katika noti zetu kwa wananchi waliotembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane jijini Mbeya.
Mkuu wa wilaya ya Muleba Dkt. Abel Nyamahanga, akipewa maelezo na Mkurugenzi wa Tawi la BoT Mwanza, Bi. Gloria Mwaikambo, alipotembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi yaliyofanyika katika viwanja vya nyamhongolo jijini Mwanza.
Mhasibu Mwandamizi kutoka Tawi la BoT Mwanza, Bw. Amon Mwambonda, akifafanua jambo kwa mwananchi aliyetembela banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi yaliyofanyika katika viwanja vya Nyamhongolo jijini Mwanza.
Meneja Msaidizi Idara ya Uchumi, Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya BoT Zanzibar, Bw. Shamy Chamicha, akitoa elimu kwa mwananchi aliyetembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane yaliyofanyika katika viwanja vya Dole, Kizimbani, Unguja.
Naibu Waziri ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Khamis Hamza Chilo, akizungumza alipotembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane yaliyofanyika katika viwanja vya Dole, Kizimbani, Unguja.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, akipewa maelezo na Meneja Idara ya Uchumi Tawi la BoT Arusha, Bw. Stanslaus Mrema alipotembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini yaliyofanyika katika viwanja vya Themi, Njiro jijini Arusha. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella wakikabidhiwa zawadi baada ya kutembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini yaliyofanyika katika viwanja vya Themi, Njiro jijini Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Bw. Peter Serukamba akipewa maelezo na Meneja Msaidizi, Idara ya Uchumi na Takwimu,Tawi la BoT Dodoma, Bi. Angella Abayo, akifafanua jambo kwa alipotembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati, yaliyofanyika viwanja vya Nzuguni, Dodoma.
Afisa wa Tawi la BoT Dodoma, Bi. Janne Bushiri, akigawa vipeperushi kwa wananchi mara baada ya kuwapa elimu kuhusu utambuzi wa alama za usalama katika noti zetu pamoja na njia sahihi za utunzaji wa noti.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, akimkabidhi Mkurugenzi wa Tawi la BoT Mtwara tuzo ya ushindi wa kwanza kwa kundi la Mamlaka za Udhibiti na Usimamizi kwenye Maonesho ya Nanenane kanda ya kusini yaliyofanyika katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.