Na Sophia Kingimali
Mkuu wa Kitengo cha Sheria kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Muhidin Mapeyo amekitaka chama cha wananchi CUF kufuata sheria na Ushauri wa kitaalamu ili kuboresha utendaji wa chama hicho
Hayo ameyasema Leo Agosti 4 jijini Dar es salaam kwenye zoezi la uhakiki wa vyama vya siasa linaloendelea nchini.
“Lengo la uhakiki huu tunataka muendelee kufanya vizuri katika chama chenu,chama chenu ni kikubwa hivyo mkifuata taratibu zilizopo mtaendelea kufanya vizuri zaidi”amesema Mapeyo.
Aidha Mapeyo ameongeza kuwa vyama vinakaguliwa ili viendelee kufanya vizuri na kujiendesha kama taasisi rasmi.
Kwa upande wao baadhi ya Viongozi Wanawake wa vyama vya siasa vya upinzani wamempongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kulea vyama vyao na kuleta maridhiano mazuri nchini.
Wamesema maridhiano hayo yameleta tija katika vyama vyao kwa kuwa na mahusiano mazuri na Serikali.
Wakizungumza Leo Agosti 4 kwa nyakati tofauti baada ya uhakiki wa chama cha CCK na CUF unaofanywa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini,ulionza juzi Mkoani Dar es Salaam,wamesema Rais Dk. Samia ameihakikishia Dunia kuwa wanawake wa Tanzania wanaweza.
“Licha ya Rais Samia kulea vyama vyetu na kuleta maridhiano lakini pia amekuwa mstari wa mbele kuwakomboa wanawake Kiuchumi”amesema Katibu wa Jumuiya ya Wanawake wa chama cha Siasa cha CCK Emmy Mwakisole .
Emmy amesema anamshukuru Rais Dk. Samia katika mambo mengi ikiwemo kuwahimiza wanawake nchini kujikwamua kiuchumi na kusonga mbele.
“Kauli yake hiyo ya mara kwa mara imetupa mwamko sisi wanawake wa CCK kupeana elimu ya kujikwamua kiuchumI”,amesema.
Naye,Mkurugenzi wa Fedha kutoka CUF Zainabu Mndolwa amesema,chama chao kimezingatia jinsia hivyo kila panapochaguliwa viongozi lazima nafasi ya mwanamke ipewe kipaumbele.
Zainabu amesema uongozi wa Rais Dk. Samia umetoa mwanya kwa wanawake wa kitanzania kuweza kuthaminiwa katika shughuli zao wanazozifanya.