Mlezi wa Kampuni ya Chilongola Agro Forest Mafinga Iringa, Mbunge wa Viti Maalamu Mkoa wa Iringa Mhe. Rita Kabati akifurahia jambo na Mkurugenzi wa kikundi cha Chilongola Agro Forest Mafinga Iringa Bw. Andrew Manifredy Salaka Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Chilongola Agro Forest Limited katikati na mmoja wa wanufaika wa kikundi hicho Joseph Kipako.
………………………………….
NA JOHN BUKUKU, MBEYA
Mkoa wa Iringa umejipanga kuanzisha shamba darasa kila halmashauri kwa ajili ya kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kufanya kilimo kinacholeta kuleta tija na kupata fursa ya kujiajiri wao wenyewe kwa ajili ya kuendesha Maisha yao.
Akizungumza Agosti 2, 2023 katika Maonesho ya Wakulima Nanenane kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Mlezi wa Kikundi cha Chilongola Agro Forest Mafinga Iringa ambacho kinajishughulisha na uandaajiwa miche ya bora ya mbegu za Parachichi, Mbunge wa Viti Maalamu Mkoa wa Iringa Mhe. Rita Kabati, amesema kuwa Mkoa wa Iringa una hali ya hewa rafiki na ardhi kwa ajili ya kilimo cha parachichi.
Mhe. Kabati amesema kuwa katika kuanzisha mashamba darasa ya Parachichi kila halmashauri watawatumia vijana wasomi wa kilimo kwa kutengeneza makundi ili waweze kuwasaidia vijana wengine katika kuhakikisha wanafikia malengo tarajiwa.
“Kikundi hiki kimeanza kuzalisha miche ya parachichi zaidi ya Laki saba, hivyo tunatarajia kuanza kuuza kila halmashauri ambayo inauzwa kati ya shilingi elfu tano mpaka elfu kumi kwa mche mmoja ” Mhe. Kabati
Amesema kuwa wakati umefika vijana kufikiria kujiajiri baada ya kumaliza masomo yao kupitia fursa ambazo zipo katika sekta ya kilimo.
Mnufaika wa Mradi wa Miche ya Parachichi Bw. Joseph Kipako, amewataka vijana kuchangamkia fursa katika sekta ya kilimo ili waweze kuondokana na utegemezi.
Bw. Kipako amesema kuwa kuna vijana wengi wamemaliza elimu ya juu lakini hawana kazi ya kufanya, hivyo wakati umefika wa kuhakikisha kilimo kinabadilisha maisha yao.
“Vijana wengi wanacheza mchezo wa kubahatisha wa kubeti bila kupata faida yoyote, naomba vijana wezangu kuacha tabia hiyo na kwenda kijishughulisha na masuala ya kilimo” amesema
Mlezi wa Kampuni ya Chilongola Agro Forest Mafinga Iringa, Mbunge wa Viti Maalamu Mkoa wa Iringa Mhe. Rita Kabati akiwa na wanakikundi wa Kampuni ya Chilongola Agro Forest Mafinga Iringa kwenye maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.
Mlezi wa Kampuni ya Chilongola Agro Forest Mafinga Iringa, Mbunge wa Viti Maalamu Mkoa wa Iringa Mhe. Rita Kabati akiwa katika picha ya pamoja na wanakikundi wa Kampuni ya Chilongola Agro Forest Mafinga Iringa kwenye kitalu cha miche ya parachichi waliyoiandaa kwa ajili ya mbegu katika maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.
Baadhi ya vitalu walivyoviotesha tayari kwa ajili ya kupanda kwenye mashamba makubwa na mashamba Darasa katika maeneo mbalimbali mkoani Iringa miche hiyo inauzwa kati ya shilingi elfu tano mpaka elfu kumi kwa mche mmoja.