Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Dkt. Eliza Mwakasangula na waandishi wa habari katika banda la chuo hicho kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Wanafunzi mbalimbali wakitembelea banda la Chuo Kikuu cha Mzumbe katika maonesho ya kilimo ya nanenane yanayofanyika kitaifa kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya kwa ajili ya kujiunga na chuo hicho kwa masomo ya taaluma mbalimbali.
…………………………………….
Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Dkt. Eliza Mwakasangula amesema kuwa Chuo hicho kimeendelea kutoa elimu Bora na inayowasaidia wanafunzi kumudu soko la ajira na kuweza kujiajiri wenyewe mara wanapohitimu masomo yao.
Ameyasema hayo Agosti 1, 2023 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya,
Amesema kuwa ushiriki wao katika Maonesho hayo ni kuhabarisha Umma juu ya huduma wanazozitoa na hasa upande wa mafunzo na kutangaza Programu zao mbalimbali zinazotolewa na Chuo hicho.
“Tupo kwenye Maonesho ya Nanenane kuzungumza na wananchi kuwaeleza Programu zetu ambazo zimekuwa zikiwasaidia sana wahitimu wetu kujitegemea kwa kujiajiri wenyewe , pia kukidhi ushindani uliopo kwenye soko la Ajira” amesema Dkt. Mwakasangula.
Kwa upande wao Baadhi ya Vijana waliotembelea katika Banda la Chuo hicho wameonesha kufurahishwa na Programu zinazotolewa na Chuo hicho na kusifu mpangilio mzima wa namna Ada za masomo zinavyopangiliwa na kugawanywa kwa muhula nakufanya ulipaji wake kuwa rahisi.