Waziri wa habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Nape Nnauye akishuhudia uzinduzi huo jijini Arusha.
Waziri wa habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Nape Nnauye akizungumza katika uzinduzi huo
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Posta Tanzania,Macrice Mbodo akizungumza katika uzinduzi huo jijini Arusha.
Julieth Laizer ,Arusha
Arusha.Waziri wa habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Nape Nnauye amelitaka shirika la posta Tanzania kuwa wabunifu katika utoaji wa huduma za bima bila kuwa na urasimu utakaomwondolea mwananchi mlolongo wa hupatikanaji wa haki yake.
Waziri Nape ameyasema hayo jijini Arusha katika hafla ya uzinduzi wa biashara ya bima ya shirika la posta ambapo amewataka kuwa wabunifu wa vifurushi vya bima vitakavyomnufaisha mwananchi wa nchi hasa waliopo maeneo ya vijijini.
“Pamoja na kuwa na ubunifu huu wa kuanzisha bima Ukiweza kumuunganisha wakulima na wafugaji kwa kuwafuata mahali walipo utakuwa umeongeza thamani ya shirika la posta Tanzania,”amesema Waziri Nnauye.
Aidha amesema kuwa katika kutoa huduma stahiki za bima kutapunguzia misongo ya mawazo wananchi wa mlolongo wa rushwa kwani hali hiyo itasaidia kuweza kujivunia na kulisemea shirika la posta Tanzania mahali popote.
“Asilimia kubwa ya wananchi waishio pembezoni mwa miji hujikita na kilimo,ufugaji na uvuvi hivyo ni lazima shirika la posta kuwa wabunifu kwa kufanya utafiti na kujikita huko ili kuongeza tija ya uwekezaji katika teknolojia za kisasa,”alisema Waziri Nnauye.
Mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Arusha ,John Mongela ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Arusha,Felician Mtahengerwa ameshukuru kuwepo kwa mabadiliko katika wizara hiyo kwani inatia moyo katika utendaji wa kazi kutokana na matumizi ya Teknolojia za kisasa(Tehama) katika kuharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Posta Tanzania,Macrice Mbodo amesema kilichopelekea kutoka katika uwakala kwenda kwenye udalali wa bima ni pamoja sheria ya bima sura ya 394 na kanuni zake kutokuruhusu ushirikiano wa kampuni zaidi tatu kutoa huduma hiyo.
“Baada ya kufuata taratibu zote zilizohitajika Aprili 17,2023 tulifamikiwa kusajili brela jina letu jipya la mshauri na dalali wa bima ya posta hali ambayo itatuwezesha kutoa huduma zetu kwa kushirikiana na makampuni zaidi ya matatu tofauti na ilivyokuwa hapo awali,”amesema Mbodo.
Kamishina wa bima Tanzania(TIRA) Dk Baghayo Saqware amesema mtandao wa shirika la posta unafahamika katika kuunga juhudi katika sekta ya fedha hususani kwenye eneo la bima jambo ambalo limeamuliwa kwa njia ya busara ili kutoa huduma hiyo kwa wananchi kikamilifu.
Dk Saqware amesema mashirika la posta duniani yanajishughulisha na biashara hiyo ya bima lakini kwa eneo la ukanda wa Afrika ya mashariki shirika la posta Tanzania limekuwa mfano wa kuigwa.
Amesema uzinduzi wa bima hiyo kupitia shirika la posta Tanzania ni ishara nzuri ya utekelezaji wa mipango ya serikali katika kuendeleza sekta ya bima nchini hivyo watatoa ushirikiano kwao ili huduma hiyo iwafikie watanzania kikamilifu na walioko pembezoni mwa miji.