MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Taifa Mohamed Ali Kawaida,akiwahutubia na kufunga mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo Vijana wa UVCCM Mkoa wa Kusini Unguja(Hawapo pichani), yaliyofanyika katika Chuo cha Mafunzo na Uongozi cha Tunguu Zanzibar.
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Mohamed Ali Mohamed (Kawaida), amesema vijana wa Chama hicho haitoshi kulinda Viongozi wao kwa maneno badala yake wajielekeze katika vitendo vinavyobeba dhamira, mikakati na ujasiri wa kuleta ufanisi ndani ya Chama na Jumuiya zake.
Kauli hiyo ameitoa katika ufungaji wa mafunzo elekezi ya Viongozi wa UVCCM Mkoa wa Kusini Unguja,yaliyofanyika katika Chuo cha Mafunzo na Uongozi kilichopo Tunguu Zanzibar.
Alisema kuwa Vijana wa UVCCM wamatakiwa kuwa imara wakati wote kwani ndio wenye dhamana kubwa ya kulinda kwa gharama yoyote maslahi ya Chama na Jumuiya zake pamoja na Viongozi wake.
Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo MCC Mohamed Kawaida, alisema historia inaonyesha kuwa Umoja huo ndio chimbuko la kuwaandaa Viongozi bora nchini walioiva kimaarifa,kiujuzi,kimaadili, uaminifu, wachapakazi na wenye uzalendo wa kweli.
“Haitoshi kusema, kuimba na kuwasifu tu Viongozi wetu badala yake tuonyeshe misimamo, dhamira, utetezi na ulinzi wetu kwa vitendo na hoja imara zinazoendana mahitaji ya siasa za Sasa. “, alisema Mwenyekiti huyo Mohamed Kawaida.
Mohamed, aliwasihi washiriki wa mafunzo hayo kutumia mbunu, maelekezo na nasaha walizopewa kuleta Mabadiliko chanya katika maeneo yao ya kiutendaji.
Pamoja na hayo alikwambia washiriki hao wa mafunzo kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa ameendelea kufanya kazi kubwa ya kufungua milango ya uwekezaji inayotoa fursa za ajira kwa vijana wa rika na fani mbalimbali nchini.
Kupitia hafla hiyo aliwasihi Vijana mbalimbali nchini kujipanga vizuri ili waweze kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za Uongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Mwaka 2025.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja huo Mussa Haji Mussa, alipongeza washiriki wa mafunzo hayo kwa nidhamu na juhudi zao katika kufuatilia mada zilizotolewa katika mafunzo.
Akisoma risala Katibu wa UVCCM Mkoa wa Kusini Unguja Mohamed Ali Mohamed, alisema mafunzo hayo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo vijana wa UVCCM Mkoa wa Kusini Unguja yamefanyika kwa ufanisi mkubwa.
Alisema katika mafunzo hayo zimetolewa mada mbalimbali zikiwemo Historia ya CCM na Jumuiya zake, muundo wa CCM na Jumuiya zake, mipaka na majukumu ya Viongozi wa CCM na Jumuiya zake, Historia ya Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Kupitia risala hiyo wamewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuimarisha Uchumi kupitia mradi wa uwekezaji katika Bandari Dar es salaam utakaotekelezwa na Kampuni ya DP World kutoka Dubai.
Jumla ya Vijana Jumla 207 wanaume 124 wanawake 83 wa UVCCM Mkoa wa Kusini Unguja wamehitimu mafunzo hayo elekezi na kutunukiwa vyeti.