Na. Dennis Gondwe, KIKUYU KASKAZINI -DODOMA.
WAKAZI wa Wilaya ya Dodoma wametakiwa kutunza na kulinda Mazingira ili kujihakikishia uhai wa maisha ya wanadamu na viumbe hai.Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipoongoza zoezi la usafi wa Mazingira na upandaji miti kuzunguka Zahanati ya Kikuyu iliyopo Kata ya Kikuyu Kaskazini jijini hapa.Shekimweri alisema kuwa uhai wa wanadamu upo kwenye mazingira safi yenye miti mizuri
. “Nisisitize mambo machache kwenye zoezi la kupanda miti. Katika uumbaji Mwenyezi Mungu ametuumba kwa kutegemeane na mazingira hakuna namna maisha yetu yatakuwepo pasina uwepo wa miti kwenye mazingira yanayotuzunguka.
Sisi tunatoa hewa inaitwa ‘carbon dioxide’ ambayo kwa uumbaji wa Mungu hiyo ndiyo hewa safi kwa miti. Na yenyewe inatoa hewa chafu ambayo inaitwa ‘oxygen’ ambayo kwa maisha ya wanadamu ndiyo hewa safi.
Kwa hiyo tunabadilishana hewa chafu kwa hewa safi” alisisitiza Shekimweri.Alikemea tabia ya kukata miti. “Sote kwa pamoja tukemee tabia ya kukata miti. Kwa maana hiyo ukiona mtu anakata mti kwa tafsiri nyepesi anakuondolea hewa safi” alisema Shekimweri
.Aliwakumbusha maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya matumizi ya nishati mbadala.
“Mhe Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliekeleza kuanzia Januari mwakani matumizi ya mkaa yatakuwa marufuku. Kila mmoja ajielekeze kwenye matumizi ya nishati mbadala. Kwa hiyo niwaombe tujielekeze kwenye nishati mbadala kwa kufuata maelekezo mema ya Mheshimiwa Rais. Kwa kufuata maelekezo hayo tulio wengi tutakuwa salama na dunia itakuwa salama.
Kwa watumishi wa umma natamani muwe wa mfano katika kuitikia maelekezo ya serikali.
Kunapokuwa hakuna wateja wa kununua mkaa maana yake hakutakuwa na mzalishaji wa mkaa” alisema.Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde aliwapongeza wakazi wa Kata ya Kikuyu Kaskazini kwa muitikio wao katika kupanda miti na kufanya usafi kuzunguka Zahanati ya Kikuyu.
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, nikushukuru sana kujumuika nasi siku ya leo kufanya usafi katika Kata ya Kikuyu Kaskazini. Niwashukuru na wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kushiri mazoezi haya.
Muitikio huu unaonesha kuwa tunaelewa manufaa ya kupanda na kutunza miti katika mazingira yetu” alisema. Aidha, aliupongeza uongozi wa Zahanati ya Kikuyu kwa kuboresha mazingira ya zahanati hiyo.
“Nitakuwa mnyimi wa fadhila nisipomshukuru sana Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kikuyu. Leo nimekuja nimeshangaa sana mazingira ya hapa. Ametufundisha jambo kwamba lazima katika maeneo yetu ya serikali tutunze na kuboresha mazingira. Zahanati ya Kikuyu inapendeza na mimi nitawaunga mkono na kuipendezesha zaidi ili iwe kati ya zahanati chache za mfano katika Jiji la Dodoma” alisema Mavunde.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Serikali ya Mtaa wa Kikuyu, Mohammed Mussa alisema “uongozi wa mtaa tunawahamasisha wananchi wote wa Kikuyu washiriki mazoezi ya usafi na upandaji miti kwa sababu usafi unatupa afya na kutufanya tuonekane wastaarabu na kudumisha mila za kitanzania.
Uchafu ni tendo baya linaleta magonjwa na kupunguza uwezo wa afya. Ukiwa huna afya huwezi kufanya shughuli zako na taifa litaathirika kwa kuwa na watu wasio na afya njema. Sambamba ya upandaji miti kwa lengo ya kutupatia hewa safi”
.Jumla ya miti 30 ya matunda, kivuli na kupendezesha madhari ilipandwa katika Zahanati ya Kikuyu katika halfa iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma na kuhudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Madiwani, maafisa waandamizi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wanavyuo, kikundi cha Kikuyu jogging na mamia ya wananchi wakereketwa wa uhifadhi wa Mazingira.