Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Taifa Daniel Chongolo akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla alipo wasili katika uwanja wa CCM kirumba uliopo Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza.
Wananchi mbalimbali kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa wakiwa katika uwanja wa CCM kirumba kwaajili ya mkutano wa Katibu Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo amesema wanaotukana juu ya uwekezaji wa bandari wasijibiwe kwa matusi bali Chama hicho kijikite kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuwanyamazisha kwa vitendo.
Chongolo ameyasema hayo leo Jumapili Julai 30, 2023 alipokuwa akizungumza na wananchi kutoka Mikoa sita ya Kanda ya ziwa katika uwanja wa CCM Kirumba uliopo Wilaya ya Ilemela Mkoani hapa.
Amesema ukosoaji huo wameuzoea kwani hata walipoanza kutekeleza miradi mikubwa ikiwamo mradi wa kufua umeme wa bwawa la Kihansi na bomba la mafuta walipingwa na watu wasio na nia njema na Taifa la Tanzania.
” Ilani ya Chama Cha Cha Mapinduzi (CCM) ni kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na kutatua kero za wananchi,ukosojai huu haujaanza leo hivyo Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuboresha mazingira mazuri kwa wananchi kwa kuwaletea maendeleo”,amesema Chongolo
Akizungumza kwenye kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu kwa namna anavyoleta fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya mendeleo kwenye Mkoa huo.
Amesema uwekezaji ni ufunguo wa fursa katika Taifa hivyo wananchi wanatakiwa kuelewa lengo la Serikali la kuwa na wigo mpana wa kuchochea maendeleo.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Atupele Mwakibete (Mb) amesema Bandari za hapa nchini hazina ufanisi unaotakiwa ndio maana wanakodisha baadhi ya magati ya Bandari ya Dar es salaam ili kuongeza ufanisi utakaoleta tija katika Taifa.
Amesema Sekta binafsi zinamchango mkubwa kwani zinachangia asilimia 90 katika pato la Taifa hivyo Serikali itaendelea kushirikiana nazo ili nchi izidi kuendelea.
Mwakibete ameeleza kuwa uwekezaji wa Bandari hiyo utakapokamilika itakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi ikiwemo ajira.