Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto) akipokea kwa niaba ya watanzania Tuzo ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuwa Taasisi Bora ya Udhibiti kwa Mwaka 2023 kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TBS, Prof. Othman Chande katika hafla iliyofanyika leo tarehe 28/7/2023 katika Ofisi za TBS Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akishika Tuzo ya kuwa Taasisi Bora ya Udhibiti kwa Mwaka 2023 Barani Afrika baada ya kukabidhiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TBS, Prof. Othman Chande katika hafla iliyofanyika leo tarehe 28/7/2023 katika Ofisi za TBS Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Prof. Othman Chande akizungumza katika hafla ya kuwasilisha Tuzo ya TBS kuwa Taasisi Bora ya Udhibiti Afrika kwa Mwaka 2023 iliyofanyika leo tarehe 28/7/2023 katika Ofisi za TBS Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa Shirika wa Viwango Tanzania (TBS) katika hafla ya kuwasilisha Tuzo ya TBS Kuwa Taasisi Bora ya Udhibiti Afrika kwa Mwaka 2023 iliyofanyika leo tarehe 28/7/2023 katika Ofisi za TBS Jijini Dar es Salaam.
………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeongeza fursa ya uwekezaji nchini baada ya kushinda Tuzo ya kuwa Taasisi Bora ya Udhibiti kwa Mwaka 2023 Barani Afrika zilizoandaliwa na Taasisi ya African Leadership Magazine ambayo imeshirikisha nchi mbalimbali kutoka Afrika.
TBS Mei 8 mwaka huu TBS iliteuliwa kati ya Taasisi mbili Barani Afrika kuingia katika ushindani wa kuwania Tuzo ya Taasisi bora ya udhibiti 2023 ya Africa Business Leader Award ambazo zimeandaliwa na Taasisi ya Africa Leadership Magazine.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam leo tarehe 28/7/2023 katika hafla ya kupokea tuzo hiyo kwa niaba ya watanzania, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa TBS wamefanya kazi kwa uweledi na kuleta heshima kubwa kwa kushinda Tuzo jambo ambalo linaleta taswira nzuri katika viwanda na Biashara.
“Wizara itaendelea kusimamia na kuhakikisha na kujenga mazingira bora na wezeshi kwa Wafanyabiashara na Wawekezaji katika Sekta ya Viwanda ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa bora za kushindaniwa katika soko la Dunia” amesema Mhe. Kijaji.
Amesema kuwa anajivunia mafanikio ya makubwa TBS kutokana yanaiweka Tanzania katika ramani ya Bara la Afrika pamoja na kuleta chagizo katika masuala ya viwango kwani ni kielelezo tosha kuwa Tanzania kuwa ni nchi yenye mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara.
“Nina imani kwamba tuzo hii itakuwa kivutio kwa bidhaa zetu kupata soko ndani na nje ya nchi, tuzo hii imekuwa ni motisha na chachu kwetu na tunaahidi kuendelea kuwatumikia wananchi na kuwahakikishia mazingira rafiki katika kuhakikisha tunaendelea kupiga hatua” amesema Dkt. Kijaji.
Mhe. Dkt. Kijaji amefafanua kuwa mafanikio ya TBS ni ishara ya juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kuna mazingira wezeshi ya biashara na yanaitangaza Tanzania katika sekta ya Viwanda na Biashara.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Prof. Othman Chande, amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suruhu Hassani kwa uongozi wake bora wenye kuleta tija.
Prof. Chande amesema kuwa Tuzo ya African Busines Leadership Awards huandaliwa na Taasisi ya African Leadership Magazine na kushirikisha makundi mbalimbali kutoka nchi tofauti Barani Afrika ambapo TBS ilitangazwa mshindi.
Amesema kuwa pamoja na ushindi wa TBS Tanzania, pia Mkurugenzi wa Mohammed Enterprises Bw. Mohammed Dewji ameshinda tuzo ya African Busines Leader of the Year 2023.
Pia Mkurugenzi Mtendaji wa Lake Oil Ally Edha Awadh ameshinda Tuzo ya Young African Energy Leader of the Year 2023 na Tanzania Portland Cement PLC iliibuka mshindi wa pili kama African Company of the Year 2023.