Na Albano Midelo,Songea
MKOA wa Ruvuma unatarajia kuzindua wiki ya unyonyeshaji wa maziwa ya
mama Duniani,Agosti Mosi,2023 katika Kituo cha Afya kata ya Ruvuma
kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Stephen ndaki amesema
Tanzania inaungana na nchi nyingine Duniani kuadhimisha wiki ya
unyonyeshaji wa maziwa ya mama ambayo itaanza Agosti Mosi hadi 7
mwaka huu.
“Lengo la kuhamasisha unyonyeshaji maziwa ya mama ni kulinda na
kuendeleza afua ya unyonyeshaji kama njia mojawapo ya kuboresha hali
ya lishe kwa watoto’’,alisisitiza Ndaki.
Hata hivyo amesema kwa mwaka huu wiki ya unyonyeshaji maziwa katika
Mkoa wa Ruvuma,itafanyika katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa
Ruvuma ambapo ametoa rai kwa viongozi,watendaji na wananchi kushiriki
kikamilifu kwenye maadhimisho hayo .
Kaulimbiu ya mwaka huu ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama
inasema “Saidia unyonyeshaji,wezesha wazazi kulea Watoto na
kufanya kazi zao kila siku’’.
Mpango Jumuishi wa Taifa wa Lishe unalenga kuweka mazingira rafiki
yanayomwezesha mwanamke kunyonyesha ili kulinda na kuendeleza
unyonyeshaji wa maziwa ya mama.
Kupitia mpango huo serikali na wadau wengine hufanya kazi pamoja
kuendeleza, kuhamasisha na kulinda unyonyeshaji watoto maziwa ya
mama ili kuimarisha afya ya jamii.
Mpango Jumuishi wa taifa wa Lishe unatambua kuwa unyonyeshaji wa
maziwa ya mama ni jukumu la pamoja linaloenda sanjari na utekelezaji wa
sera mbalimbali za nchi zinazosaidia kuboresha afya ya mtoto na jamii kwa
ujumla.