TABORA
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dkt. Batlida Buriani ameupongeza ugeni wa watu 10 kutoka nchini Afrika Kusini uliokuja kujifunza kuhusu ufugaji nyuki huku akisema ujio wao utasaidia kuimarisha biashara ya ufugaji nyuki baina ya Tanzania na nchi hiyo.
Akizungumza katika hafla ya kuwaaga wageni hao iliyofanyika mkoani Tabora, Balozi Dkt. Burian amesema, ugeni huo una faida kwa Tanzania kwani utachochea mahusiano mazuri kwenye eneo la ufugaji nyuki pamoja na kuitangaza asali ya Tanzania Kimataifa kwani wamevutiwa ubora wa asali hiyo
“Tanzania na Afrika Kusini ni ndugu na Sisi tutaendelea kuimarisha mahusiano yaliyojengwa na Waasisi wetu wa nchi hizi mbili kwa kuhakikisha ufugaji wa nyuki unakuwa endelevu kwetu sote “amesema Dkt. Batilda
Aidha, amesema mkoa umefarijika na ugeni huo ambao utawawezesha wafugaji nyuki kunufaika na masoko ya kimataifa.
“Namshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa kuendelea kuifungua Tanzania kimataifa na hii kwetu Tabora ni fursa ya kunadi asali yetu .” ameongeza.
Kwa upande wake Kiongozi wa Wajumbe hao ambaye ni Mkuu wa Idara ya Kilimo na Maendeleo Vijijini Kaskazini Magharibi mwa Afrika Kusini, Zakaria Thupi ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya ufugaji nyuki
Ameongeza kuwa Afrika Kusini inajihusiha na masuala ya ufugaji nyuki lakini Tanzania imepiga hatua zaidi ukilinganisha na nchini kwao
” Tumepata elimu ya kutosha, Tutakaporudi nyumbani tutaishauri Serikali yetu kuimarisha ushirikiano wa dhati na Tanzania katika suala zima la ufugaji nyuki, huu ni mwanzo tu wa ushirikiano wetu kwenu katika suala zima la ufugaji nyuki” amesema Thupi
Naye, Mkurugenzi wa Utafiti wa Ufugaji Nyuki kutoka Taasisi ya Utafiti ya Misitu Tanzania (TAFORI), Allen Kazimoto ameushukuru Uongozi wa Mkoa wa Tabora kwa kwa ushirikiano walioupatia huku akisisitiza kuwa ziara hiyo itakuwa ni mwanzo wa ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na Afrika Kusini.