Wizara za Kisekta zimekutana leo Julai 28,2023 jijini Dodoma kwa lengo la kujadili Mpango Kazi wa Kuongoa Shoroba za Wanyamapori nchini ikiwa ni mkakati maalum ndani ya Serikali wa kupunguza athari za wanyamapori wakali na waharibifu kwa wananchi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kikao ambaye ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu),Bw. Anderson Mutatembwa amesema kuwa Wizara za Kisekta zimepata uelewa wa pamoja kuhusu Shoroba za Wanyamapori.
“Nina imani kupitia kikao hiki tutapata uelewa wa pamoja na itasaidia katika mipango na utekelezaji wa miradi yetu yote kwenye Wizara zote za Kisekta, moja tutakuwa tumeshafahamu shoroba ni nini na pale tunapokuwa na mashaka tukawasiliana na Wizara ya Maliasili na Utalii ” alisema Mutatembwa.
Amefafanua kuwa changamoto ya kuvamiwa kwa maeneo ya Shoroba za Wanyamapori ni suala mtambuka linalogusa Wizara mbalimbali za Kisekta akitolea mfano wa TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Amesema baadhi ya Shoroba ziko kwenye maeneo yaliyohifadhiwa ambayo nayo pia yamevamiwa kutokana kutokuwepo kwa uratibu ndani ya Serikali hivyo kikao hicho kitatatua changamoto hiyo.
Amesema kuwa kuna maeneo ya shoroba ambayo ndani yake kuna vijiji ambavyo vimesajiliwa na TAMISEMI, mengine yapo ambayo yana wawekezaji ambao wamepewa mashamba na Wizara ya Ardhi.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamishna Benedict Wakulyamba amesema matarajio ya kikao hicho ni kuboresha masuala ya uhifadhi na utalii na kwamba kila Wizara na kila Sekta ina jukumu la kufanya shughuli za uhifadhi na kuboresha masuala ya utalii kwa ujumla.
Aliongezea kuwa, baada ya maeneo ya shoroba kufanyiwa tathmini endapo yataonekana kutokuwa na sifa ya kuwa Shoroba shughuli za wananchi zitaendelea kufanyika kama kawaida.
Kwa upande wake Mtafiti Mkuu Wanyamapori, kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Dkt. Hamza Kija amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori iliainisha takribani Shoroba 61 nchini ambapo kati ya hizo zikachaguliwa shoroba 20 za kipaumbele kutokana na umuhimu wake kiikolojia,kiuchumi, kisiasa, na umuhimu katika shughuli za utalii.