Na. Mwandishi Wetu-DSM.
Kufuatia Aumzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kuunda Wizara mpya ikiwemo ile ya Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji na Kumteua Profesa Kitila Mkumbo kuwa Waziri wa Wizara hiyo, leo Julai 28, 2023, pameshuhidiwa makabidhiano Kati Waziri Prof Mkubo akipokea kipande cha Uwekezaji kutoka kwa Waziri Dkt.Ashatu Kijaji.
Katika Makabidhiano hayo ambayo yamefanyika katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Jijini Dar es Salaam, Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa amepokea masuala manne ambayo ataendelea kuyatekeleza kwa kasi ili kuwezesha wawekezaji kuvutiwa kuja kuwekeza nchini.
“Kufuatia auamzi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, wa kuunda Wizara mpya ya Mipango na Uwekezaji, leo Waziri wa Viwanda na Biashara amenikabidhi kipande cha Uwekezaji ambacho kilikuwa chake na amenikabidhi mambo manne ikiwemo Mchakato wa Mabadiliko ya Sera ya uwekezaji ya mwaka 1996, amenikabidhi Sheria Mpya ya Uwekezaji na Kanuni zake ya mwaka 2022 ambayo ilipitishwa Bungeni hivi karibuni”, Prof. Kitila Mkumbo.
Prof. Kitila Mkumbo alisema kuwa katika makabidhiano hayo pia amekabidhiwa Bajeti ya mwaka 2023/2023 kwenye kipande cha uwekezaji akibainisha kuwa jukumu la Wizara hiyo ni kuvutia wawekezaji ili kukuza uchumi wa nchi
Aidha, Prof. Kitila amesema kuwa Wizara hiyo ina jukumu kubwa ambalo ni kuendelea kuvutia wawekezaji wakubwa kutoka sehemu mbalimbali duniani na kutoka ndani ya nchi, huku akitaja Utulivu na Utashi wa kisiasa pamoja na mazingira mazuri ya kisheria ni mambo ambayo yanavuta wawekezaji wengi kutoka nje ya nchi.
Kwa Upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji alisema kuwa tangu apatiwe kipande cha uwekezaji hapo januanri 2022 wameweza kusajili miradi 522 katika sekta mbalimbali hapa nchini.
“Kwa mwaka uliopita tangu nimeaminia na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na kupewa kipande hiki cha uwekezaji tumesajili miradi 522 kuanzia januari 2022 mpaka sasa hapa ninapokukabidhi sekta hii ambayo ni muhimu kwa nchi.
Dkt. Kijaji alisema kuwa usajili wa miradi hiyo utawezesha upatikanaji wa ajira 72,000 na kupunguza changamoto ya ajira nchini lakini pia katika uwekezaji huo nchi itapata mapato na kuunua uchumi wa Watanzani.