Na John Mapepele
JESHI la Uhifadhi litaanza rasmi kulinda ofisi zote za Wizara ya Maliasili na Utalii kuanzia Agosti 1 mwaka huu.
Kamishina Msaidizi, Ignas Kapalata ambaye ni Mkurugenzi Kitengo Cha Uratibu Jeshi la Uhifadhi, Wizara ya Maliasili na Utalii ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa askari 42 wa jeshi hilo ambazo watashiriki katika ulinzi wa ofisi za wizara.
Kapalata amesema mafunzo hayo ni ya kawaida yenye lengo la kuwakumbusha askari hao kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.
“Kama sote tujuavyo kuwa elimu haina mwisho. Tumeona ni vema kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yao kuanzia Agosti 1 mwaka huu ni bora tuwakumbushe maadili ya kazi na pia wahakikishe wanatekeleza majukumu yao kwa kutumia Sheria, kanuni na taratibu mbalimbali,’ amesema na kuongeza kuwa wameamua kutoa mafunzo hayo kama Jeshi la Uhifadhi wanyama pori na misitu.
Amefafanua kuwa askari hao wamehamishwa kutoka katika taasisi nne za wizara ambazo ni Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro, Wakala wa huduma za misitu (TFS) na Mamlaka ya Wanyapori Tanzania (TAWA).
“Jumla ya askari 42 wa Jeshi la Uhifadhi wamehamishiwa Dodoma kwa ajili ya kuanza kutekeleza malindo katika ofisi za wizara zilizoko Mtumba, Swagaswaga na zile zilizoko Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM),” ameongeza Kamishina Kapalata na kusema awali ofisi za wizara zilikuwa zinalindwa na askari wa SUMA JKT.
Amesema hatua ya kutumia askari wa jeshi la Uhifadhi imekuja baada ya taratibu za kuanzisha jeshi hilo kukamilika.
“Tunaendelea kulijenga jeshi hili taratibu ambapo moja ya eneo ni pamoja na ofisi zetu za wizara kulindwa na askari wetu,” amesema.