Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba akifanya ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Sekta ya Nishati na Viwanda Zanzibar linalofanyika tarehe 26 na 27, Julai, 2023 mjini Unguja, Zanzibar . PICHA NA Dorina G. Makaya.
Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Suleiman Masoud Makame akizungumza machache wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba, kuzungumza na wadau wa mafuta na gesi katika Kongamano la Kimataifa la Sekta ya Nishati na Viwanda Zanzibar linalofanyika tarehe 26 na 27, Julai, 2023 mjini Unguja, Zanzibar. PICHA NA Dorina G. Makaya.
Wadau wa mafuta na gesi wakifuatilia Kongamano la Kimataifa la Sekta ya Nishati na Viwanda Zanzibar linalofanyika tarehe 26 na 27, Julai, 2023 mjini Unguja, Zanzibar. PICHA NA Dorina G. Makaya.
Mhandisi Mkuu eneo la Mafuta na Gesi wa Wizara ya Nishati Mha. Joyce Kisamo akichangia mada wakati wa Kongamano la Kimataifa la Sekta ya Nishati na Viwanda Zanzibar linalofanyika tarehe 26 na 27, Julai, 2023 mjini Unguja, Zanzibar. PICHA NA Dorina G. Makaya.
Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba akisalimiana na watendaji wa Wizara ya Nishati wakati alipowasili katika ukumbi wa Mikutano wa Golden Tulip Kufungua Kongamano la Kimataifa la Sekta ya Nishati na Viwanda Zanzibar linalofanyika tarehe 26 na 27, Julai, 2023 mjini Unguja, Zanzibar. PICHA NA Dorina G. Makaya.
Wasanii wa kikundi cha Ngoma ya Kibati cha magereza wakitoa burudani.
Na Dorina G. Makaya- Zanzibar.
Waziri wa Nishati January Makamba, amewasihi viongozi kutoa taarifa sahihi kwa wananchi na kuwapa matumaini sahihi kuhusu uwezekano wa upatikanaji wa rasilimali za Mafuta na Gesi ili kuepuka taharuki inayoweza kutokea kwa wananchi pale itakapotokea kukosekana kwa rasilimali wanazotarajia.
Hayo yamesemwa tarehe 26 Julai, 2023 Mjini Unguja, Zanzibar, na Waziri wa Nishati, January Makamba wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Sekta ya Nishati na Viwanda Zanzibar linalojulikana kwa Lugha ya Kiingereza (Zanzibar Energy and Industrial Summit -ZEIS)Amesema, upatikanaji wa Mafuta na Gesi ni zoezi lenye mchakato mrefu kuanzia taratibu za majadiliano na makubaliano, leseni ya utafutaji hadi kufikia upatikanaji wa mafuta na linahitaji muda na kuwataka Wazanzibari kuvuta Subira wakati Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inalifanyia kazi jambo hili.
Waziri Makamba ameeleza kuwa, katika Kongamano hilo, Tanzania Bara imeelezea walichojifunza Bara kuhusu Majadiliano ya kufikia makubaliano ya utafutaji na uchimbaji wa Gesi na Mafuta na mambo ya kutahadhari na pia subira inayotakiwa, matayarisho na utayari wa Serikali, Rasilimaliwatu, na mfumo mzima wa Serikali wa kusimamia utekelezaji.
Waziri Makamba ameeleza zaidi kuwa, mkutano huo pia umezungumzia juu ya umuhimu wa Sekta ya Mafuta na Gesi kutoingiliwa na siasa kwa sababu wawekezaji huwa wanatazama kama kuna muafaka katika nchi husika kuhusu namna wanavyotaka rasimilimali zitumike.
Amesema, endapo ikionekana kwa wawekezaji kuwa uwekezaji wakati mwingine utatumika kama sehemu ya siasa, basi mara nyingi inakuwa ni vigumu kuwekeza katika eneo hilo.
Aidha, Waziri Makamba amesisitiza kuwa, uwekezaji wa Gesi na Mafuta una gharama kubwa na hauna uhakika sana, kwa sababa mwekezaji anaweza kutumia fedha nyingi sana kutafuta mafuta na Gesi na asiyapate hivyo muundo na mfumo wa makubaliano ni lazima uzingatie uhalisia huo ya kwamba ni teknolojia ya juu, ni mtaji mkubwa vinavyotumika na na upatikanaji wake si wa uhakika.Waziri Makamba amesema uwepo wa Taasisi kutoka Tanzania Bara, zikiwemo, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati (EWURA) katika Kongamano hilo, unaelezea na kunaonyesha ushirikiano wa hali ya juu baina ya Pande mbili za Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar kwenye eneo la Nishati.Amesema, katika Kongamano hilo, wameeleza kwa ujumla nafasi ya Nishati katika maendeleo ya nchi, umuhimu wake na wamezunguzia pia kwa undani kuhusu Mafuta na Gesi, kwani Zanzibar tangu 2016 imetunga Sheria yake ya Gesi na Mafuta hivyo kumekuwa na matumaini makubwa kuhusu upatikanaji, utafutaji na utunzaji wa Gesi na Mafuta na mchango wa Sekta ya Mafuta na Gesi kwa Maendeleo ya Zanzibar na kuwa, ni jambo jema kwamba kuna dalili na viashiria vya upatikanaji wa gesi.
Amesema, awali, suala hilo lilikuwa linasimamiwa na Serikali ya Muungano, na kuwa mwaka 2022, Waziri wa Nishati, January Makamba, aliwakabadhi Wizara ya Nishati Zanzibar taarifa zote ambazo zinahusu upande wa Zanzibar ili iwe rahisi kwa Zanzibar kukaribisha wawekezaji ili kuweza katika kutafuta mafuta na Gesi.
Waziri makamba ameeleza zaidi kuwa, Zanzibar ikipata Gesi, wakati huo Tanzania Bara ina Gesi, itakuwa ni jambo bora kabisa na litabadilisha uchumi na maisha ya watu wa nchi husika.Amesema ni muhimu kuharakisha uwekezaji kutokana na mwelekeo wa dunia kwenye Nishati mpya ambazo ni jadidifu hivyo, ucheleweshaji wa uwekezaji kwenye Nishati za mafuta na Gesi kunaweza kupelekea changamoto ya upatikanaji wa wawekezaji kwa wakati.
Akijibu swali, ni kwa kiasi gani Zanzibar inahitaji kuelekea katika uwekekezaji katika Bahari, Waziri Makamba amesema, maeneo ya Bahari yanayomilikiwa na Tanzania na nchi nyingine za Afrika yaliyofanyiwa utafiti, ni asilimia ndogo sana iliyofanyiwa utafiti ikilinganishwa na maeneo mengine duniani.
Naye Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Suleiman Masoud Makame, amesema, moja ya Azma ya mkutano huo ni kuitangaza Zanzibar kwenye suala zima la Mafuta na Gesi na kuwa mkutano huo unakwenda sambamba na utangazaji wa maeneo ya uwekezaji wa mafuta na Gesi ambayo yako tayari kwa uwekezaji.
Amesema, Maelekezo ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni Kwenda kwa kasi zaidi na jitihada zinafanyika katika kulitimiza hili ili wawekezaji wajitokeze kuwekeza katika utafutaji wa Mafuta na Gesi na tayari kampuni tano zimeonyesha nia ya kuja kufanya uwekezaji katika eneo hilo.
Ameongeza kuwa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itahakikisha kuwa Kampuni watakayofanya nayo kazi ni Kampuni yenye uwezo.Kongamano hilo la siku mbili la Kimataifa linalofanyika tarehe 26 na 27 Julai, 2023, la Sekta ya Nishati na Viwanda Zanzibar, limeshirikisha zaidi ya nchi tisa zikiwemo Marekani, Uingereza, Ujerumani, China, Uturuki, Afrika ya Kusini na Bulgaria.