Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara,Viwanda na Kilimo TCCIA Mkoa wa Mwanza Gabriel Mugini (kulia) akizungumza wakati wa kutoa taarifa ya kuanza kwa maonesho ya biashara ya Afrika Mashariki.
Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara,Viwanda na Kilimo TCCIA Mkoa wa Mwanza Gabriel Mugini akitoa taarifa ya kuanza kwa maonyesho ya biashara ya Africa Mashariki Agosti 25,2023 kwa waandishi wa habari
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Zaidi ya washiriki 400 kutoka ndani na nje ya nchi wamethibitisha kushiriki kwenye maonesho ya 18 ya biashara ya Afrika Mashariki yanayotarajia kufanyika Agosti 25 hadi Septemba 3 mwaka huu.
Hayo yameelezwa leo Julai 26, 2023 na Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara,Viwanda na kilimo (TCCIA) Mkoa wa Mwanza Gabriel Mugini, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya maonyesho hayo yatakayofanyika katika uwanja wa Furahisha uliopo Wilaya ya Ilemela Mkoani hapa.
Mugini Amesema malengo ya Maonesho hayo ni kufungua fursa kwa wafanyabiashara wa Kanda zote ili kuweza kukuza uchumi wa Taifa.
“Maonesho haya yanatoa fursa kwa Makampuni mbalimbali Afrika Mashariki ikiwemo kujitangaza, Wafanyabiashara kuongeza mtandao wa biashara,kuongeza ubora wa bidhaa na kuboreshs teknolojia,kutafuta wabia wapya wa kibiashara pamoja na kufanya utafiti wa masoko”, amesema Mugini
Kwa upande mwingine ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Kanda ya ziwa na wananchi kwa ujumla kutembelea maonesho hayo ili waweze kujifunza na kujipatia bidhaa mbalimbali.
Katika maonesho hayo mgeni rasmi anatarajia kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Ashatu kijaji huku kauli mbiu ikiwa ni “Mazingira bora ya Biashara ni kivutio cha kukuza uwekezaji wa biashara viwanda na kilimo Tanzania, Afrika mashariki na Afrika”.