MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa ukumbi wa CCM Mkoa wa Mara.
Kinana, ameweka jiwe hilo la msingi leo Septemba 26,2023 ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake akikagua miradi na utekekezaji wa ilani ya Chama hicho.
Akizungumzia mradi huo, Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Langaeli Akyo amesema hadi kukamilika kwake utagharimu sh milioni 658.
Amesema, asilimia 70 ya fedha hiyo tayari imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya ujenzi huo Mwita Gachuma ‘Mzee Gachuma’ akisaidiwa na wanachama wengine tisa.
“Mh. Makamu Mwenyekiti, Mkoa wa Mara una wanachama wengi wa CCM wenye uwezo, kama tutashirikiana pamoja hili jengo litaisha bila shida.” Amesema Akyo.
Amesema, mradi huo wa ukumbi utakapokamilika utawezesha kufanyika Kwa vikao vya Chama hicho na pia kuukodisha kwa ajili ya sherehe mbali mbali.
Aidha, baada ya kuweka jiwe la msingi, Kinana hakuongea na badala yake aliwataka viongozi wa CCM Mkoa wa Mara na Wajumbe wa Halmashauri wa Chama hicho kuzungumza nao katika kikao cha ndani, kinaendelea muda huu.