Na Jacquiline Mrisho MAELEZO
Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema, nchi ya Tanzania itakuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa maazimio yatakayotokana na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Mtaji wa Rasilimali Watu unaoendelea kufanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili kuanzia leo Julai 25 na 26, 2023.
Tanzania tutakuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunasimamia utekelezaji wa maazimio yatakayotokana na mkutano huu, maazimio yanayolenga kuimarisha rasilimali watu suala ambalo linaleta tija kwenye maendeleo ya nchi yetu kwani watu ni rasilimali muhimu kuliko zote, amesema Msigwa.
Msigwa amefafanua kuwa, mkutano huo ni wa kwanza kwa Afrika na kwa mara ya kwanza unafanyikia nchini Tanzania ambapo mwisho wa mkutano huo litatoka Azimio la Dar es Salaam ambalo ni jambo muhimu kwa nchi ya Tanzania kwani nchi za Afrika zitakapokuwa zinajadili kuhusu masuala ya rasilimali watu barani Afrika, rejea itakuwa kwenye azimio la Dar es Salaam ambalo limefanyika nchini Tanzania.
Ameendelea kueleza kuwa, nchi ya Tanzania inatekeleza miradi mingi ya maendeleo, miradi hii inaleta manufaa mbalimbali ikiwemo manufaa ya mradi wenyewe, kupata ujuzi unaotokana na teknolojia inayotumika pamoja na kubadilishana kwa teknolojia katika miradi hiyo, hivyo mkutano huo unapofanyika na maazimio yatakayowekwa kuhusiana na namna ambavyo Afrika inaweza kuendeleza rasilimali watu, Watanzania watakuwa ni wanufaika wakubwa kwa sababu wanahitaji kuwa na watu wenye ujuzi na taaluma itakayowawezesha kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Tumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mkutano huu kufanyika hapa nchini kwa sababu kufanyika kwake hapa, pamoja na yale yanayozungumzwa kwenye mkutano, uchumi wetu utaongezeka kwani washiriki wengi wataenda kutalii katika maeneo yetu na habari za mkutano huu zitasambaa duniani kote hivyo kutuletea wawekezaji zaidi na kupanua biashara zetu na nchi mbalimbali za dunia nzima amefafanua Msigwa.