Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga amekutana na ujumbe kutoka Wizara ya Madini na Maendeleo ya Migodi ya Jamhuri ya Zambia katika ziara inayolenga kujifunza mifumo ya usimamizi wa Sekta ya Madini hususan kwenye shughuli za uchimbaji wa madini zinazofanywa na wachimbaji wadogo jijini Dodoma
……..
Sekta ya Madini nchini Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kwa nchi nyingi za Afrika kwa namna ilivyoweza kurasimisha sekta ndogo ya uchimbaji madini na hivyo kupelekea wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kupitia mfumo ulio rasmi ambapo Serikali inaweza kufuatilia shughuli zao mpaka hatua ya kuuza madini yao, kupitia katika masoko ya madini yaliyopo nchini.
Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga Julai 24, 2023 jijini Dodoma alipokutana na ujumbe kutoka Wizara ya Madini na Maendeleo ya Migodi ya Jamhuri ya Zambia katika ziara inayolenga kujifunza mifumo ya usimamizi wa Sekta ya Madini hususan kwenye shughuli za uchimbaji wa madini zinazofanywa na wachimbaji wadogo.
Dkt. Mwanga amesema kuwa, uwepo wa masoko ya madini umewezesha wachimbaji kupata soko la uhakika pamoja na kuongeza mapato kutoka Sekta ya Madini na mchango wa sekta kwenye Pato la Taifa umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka 2022 umefikia asilimia 9.1 ikiwa lengo ni kufikia mchango wa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
Naye, Meneja wa Biashara kutoka Tume ya Madini George Kaseza, ameueleza ujumbe huo kuwa, hadi sasa kuna Masoko ya Madini 42 na Vituo vya ununuzi wa madini 94 katika maeneo mbalimbali yenye shughuli za uchimbaji madini.
“Uwepo wa masoko ya madini umeongeza mapato kutoka shilingi bilioni 8.30 Mwaka wa Fedha 2018/19 hadi kufikia shilingi bilioni 157.43 Mwaka wa Fedha 2022/23,” amesema Kaseza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Wizara ya Madini Zambia Samson Phiri amesema mafunzo hayo nchini yamelenga kuwawezesha wataalam wa Sekta ya Madini nchini Zambia kujifunza mifumo ya usimamizi wa Sekta hiyo hususan kwenye shughuli za uchimbaji wa madini zinazofanywa na wachimbaji wadogo.
Ujumbe huo unatarajia kutembela Soko la Madini Mkoa wa Shinyanga, Soko la Dhahabu mkoa wa Geita ili kujifunza namna biasharaya madini inavyofanyika katika masoko hayo.
Ziara ya Zambia nchini inakuja ikiwa zimepita siku chache tangu ujumbe kutoka nchi ya Kenya ukiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini na Uchumi wa Bluu wa nchi hiyo Elijah Mwangi kufika nchini kujifunza kuhusu namna bora ya usimamizi wa Sekta ya Madini.