Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Willbroad Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani ) juu ya kuvikumbusha vikundi vya mchakamchaka kujisajili kwenye ofisi za Utamaduni.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Willbroad Mutafungwa akizungumza namna walivyofanikiwa kumkamata Oswald Kaijage dereva aliyetoroka baada ya kusababisha ajali.
……..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Vikundi vya mchakamchaka (JOGGING) vimetakiwa kusajiri vikundi vyao kwenye ofisi za Utamaduni katika ngazi za Wilaya na Jiji ili wapewe maelekezo ya namana ya kufanya mazoezi kwa kuzingatia usalama wao na watu wengine.
Rai hiyo imetolewa leo Ijumatatu Julai 24, 2023 na kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Willbroad Mutafungwa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya kukamatwa kwa Oswald Kaijage ambae ni dereva aliyetoroka baada ya kusababisha ajali eneo la lumala katika Barabara ya Kiseke Wilayani Ilemela siku ya Jumamosi Julai 22 mwaka huu.
Kamanda Mutafungwa amesema ajali hiyo ilihusisha gari yenye namba za usajili T.476 DZL aina ya Toyota Hilux Double Cabin kwa kuwagonga watu waliokuwa wanafanya mazoezi ya mchakamchaka katika Barabara hiyo na kusababisha vifo vya watu sita na majeruhi 16.
” Majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospital ya Mkoa Sekoutoure na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ambapo hadi sasa waliobaki katika Hospitali hizo ni watu 9″, amesema Kamanda Mutafungwa
Mwisho amevikumbusha vikundi hivyo kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi katika Wilaya husika endapo watahitaji kutumia barabara wakati wa mazoezi yao ili askari wa usalama barabarani waweze kusimamia usalama wao na watumiaji wengine ambao kwa wakati huo watakuwa wanatumia barabara hizo ili kuepusha ajali.