Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya kuhakikisha kunakuwa na ustawi wa afya ya mama na mtoto ikiwemo mpango wa Mama Samia Mentorship Program.
Amesema kuwa mpango huo ni mahsusi kwa mafunzo ya muda mfupi kazini kwa madaktari bingwa na wakunga ili waweze kuimarisha utoaji huduma kwenye Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya.
Amesema hayo leo (Jumapili, Julai 23, 2023) aliposhiriki katika mbio za NBC ‘NBC Marathon’ zilizofanyika jijini Dodoma.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa mpango mwingine wa Serikali ni kuongeza wigo wa kutoa huduma za kupima dalili za awali za saratani ya uzazi kutoka Vituo vya Afya 925 vilivyopo hadi kufikia vituo vya Afya 1,025 hapa nchini.
“Mwingine ni kuimarisha wigo wa kutoa huduma za watoto wachanga kwa ujenzi wa wodi maalum, kununua vifaa tiba na mafunzo kwa watumishi kutoka hospitali 175 hadi kufikia hospitali 275 katika mwaka 2023/2024”.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na sekta binafsi zenye lengo la kuinua michezo kama wanavyofanya NBC.
“Suala hili lipewe kipaumbele kwani sote tunatambua kuwa michezo ni zaidi ya burudani na inachangia ajira na huduma za afya nchini”
Mbio za NBC kwa mwaka 2023 zinatarajia kukusanya Sh. milioni 300 ambazo zitatumika kuboresha afya ya mama na mtoto, kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa taaluma ya ukunga nchini ili kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa uzazi.
Naye, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa michezo ni nyenzo ya mabadiliko kwa jamii katika kuelimisha, kuimarisha afya na mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya
“Tutaendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi na milango ya wizara ipo wazi. Lengo ni kupunguza wagonjwa wanaolazwa hospitali kwa kuhamasisha Watanzania kushiriki kwenye michezo ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza”