Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Mipango, Fedha na Utawala), Profesa Wineaster Anderson akipata maelezo kutoka kwa Rose Joseph Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Chuo Kikuu cha UDOM wakati alipotembelea katika banda la Chuo hicho katika maonesho ya vyuo Vikuu na taasisi za Elimu ya juu yaliyomalizika Julai 22,2023 Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
……………………………….
Na John Bukuku, Dar es Salaam
Chuo Kikuu cha Dodoma kimesema kitaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kufanikisha miradi ya maendeleo ukiwemo ule wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) ambao ni maalumu kwa vijana.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 22,2023 wakati wa kufungwa maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Mipango, Fedha na Utawala), Profesa Wineaster Anderson, amesema wanajivunia kwa chuo hicho kushiriki katika mradi huo kwa ushauri wa kitaalam.
“Tumeshiriki kikamilifu katika mradi huu, wapo wataalam wetu ambao walihusika kutoa ushauri wa kitaalam na lengo letu ni kuendelea kushirikiana na Serikali katia kufanikisha miradi mbalimbali,” amesema Profesa Wineaster.
Kwa mujibu wa Profesa Wineaster, Udom kinazalisha maarifa mbalimbali pamoja na kufanya tafiti na kuibua bunifu kwa lengo la kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Mradi wa BBT ulizinduliwa Machi,2023 ambapo vijana 812 walichaguliwa kujiunga.
Chuo hicho chenye wanafunzi zaidi ya 30,000 kinafanya vizuri katika maeneo mbalimbali kama vile Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kimekuwa kikishinda mashindano mbalimbali kitaifa na kimataifa.
Katika maonesho ya mwaka huu Udom wameyatumia kutoa elimu kwa Watanzania hasa kuhusu fursa zinazopatikana katika chuo hicho pamoja na machapisho mbalimbali.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Mipango, Fedha na Utawala), Profesa Wineaster Anderson akisalimiana na Charles Nduku mtunzi wa vitabu wakati alipotembelea katika banda la UDOM katika maonesho ya Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu yaliyofanyika Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam na kumalizika Julai 22,2023.