Na. WAF – Dar es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Afya imedhamiria kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) katika kupambana na kutoa elimu juu ya masuala ya Afya ya Uzazi Mama na Mtoto.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo Julai 22, 2023 wakati akizindua rasmi Utafiti wa Haki ya Afya ya Uzazi kwa Wanawake wa Mjini na Vijijini Kupitia Vyombo vya Habari Jijini Dar es Salaam.
“Tunataka tushirikiane kwa pamoja kati ya Serikali na TAMWA juu ya masuala haya ya Afya ya Uzazi Mama na Mtoto kwa kutoa elimu sahihi kwa wananchi ili waweze kujikinga na mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya zinaa”, amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amesema tafiti hiyo imesaidia kupata Takwimu sahihi ambapo asilimia 81 ya Wanawake wajawazito wanajifungua katika vituo vya kutolea huduma za Afya kwa kuwa wanaimani na vituo hivyo.
Amesema, matokea ya wanawake kujifungua kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya ni pamoja na kupungua kwa vifo vya watoto chini ya miaka Mitano kutoka vifo 67 katika kila vizazi hai 1,000 hadi vifo 43.
“Lakini pia, vifo vya watoto chini ya umri wa mwaka Mmoja vimepungua kutoka vifo 43 katika kila vizazi hai 1,000 hadi vifo 33”, amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha huduma za Afya ya uzazi na kuwalinda wasichana, wanawake na watoto kutokana na unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto.
“Katika juhudi hizi tunazofanya pia, tumefanikiwa katika Afya ya Uzazi kwa kupunguza kiwango cha mimba za utotoni kutoka asilimia 27 ya mwaka 2015/16 hadi asilimia 22 kwa mwaka 2022”. Amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amewataka wataalam wa Afya ya Uzazi mama na Mtoto kuvitumia vizuri vyombo vya habari kwa kutoa elimu kuhusu Afya ya uzazi kwa watoto wetu lakini tuzingatie mila zetu, desturi na taratibu za Kitanzania.
“Wataalam wangu tutumie vizuri vyombo vya habari mjipange na mkialikwa mtoe ushirikiano mzuri, mtoe elimu kuhusu Afya ya Uzazi ili tuweze kupunguza mimba za utotoni na Magonjwa ya zinaa ikiwemo UKIMWI”. Ameongeza Waziri Ummy.
Utafiti huo umelenga kutoa takwimu za msingi zinazohitajika kwa mradi wenye mada isemayo “Uchechemuzi kupitia vyombo vya habari Vijijini na Mjini kwa Wanawake na Wasichana katika Haki za Afya ya Uzazi wa Kijinsia nchini Tanzania.