Na. Dennis Gondwe, IPAGALA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma kupeleka timu ya maafisa mazingira na afya kufanya ukaguzi katika maeneo ya Mtaa wa Ipagala kukagua hali ya usafi wa mazingira kutokana na changamoto wa baadhi ya wakazi wa maeneo hayo kutojitokeza kufanya usafi wa mazingira.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Usafi na uthibiti wa taka ngumu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alipokuwa akiongea na mamia ya wakazi wa Kata ya Ipagala waliojitokeza katika usafi wa pamoja kwenye korongo la kitaa cheusi.
Kimaro alisema “kwa sababu eneo hili lina changamoto ya wananchi kutojitokeza kufanya usafi katika maeneo yao. Wananchi wanalalamika kuwa watu wanaokaa kwenye nyumba zenye mageti hawajitokezi kufanya usafi na kuwaanchia wanaoishi katika nyumba zisizo na mageti kufanya usafi.
Nimetoa maelekezo kwamba wiki ijayo kuanzia siku ya Jumatatu timu ya maafisa afya na mazingira watapita nyumba kwa nyumba kuhamasisha usafi na ambao watakaidi tutachukua hatua kwa mujibu wa sheria”.
Akiongelea zoezi la usafi wa pamoja, alisema kuwa usafi wa pamoja ulifanyika katika Kata ya Ipagala na Kizota. “Kwa wiki hizi mbili tumeweka nguvu zaidi na kushiriki sisi wenyewe viongozi kwa Kata ya Ipagala na Kizota ambapo tulibaini kuna baadhi ya maeneo ambayo ni machafu na wananchi hawajitokezi kufanya usafi.
Leo tumekuwa katika eneo la Sulungai na Ipagala katika Korongo la Kitaa cheusi. Tumegundua wananchi wanatupa taka ovyo na tumekuta wananchi wanatupa hata pampasi” alisema Kimaro.
Alisema kuwa kuna wakati vikundi vya kijamii ambavyo vimepewa jukumu la kukusanya taka nao wanazitupa katika kongongo hilo. “Tumehamasisha wananchi na kujitokeza kufanya usafi katika korongo hili na wiki iliyopita tulifanya usafi eneo hilo. Tumetoa maelekezo kwa wananchi wote kujiepusha na tabia ya kutupa taka ovyo kwasababu usafi ni ustaarabu na unaanza na sisi wenyewe” alisema Kimaro.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Ipagala, Elenei Mogwa aliwashukuru wananchi waliojitokeza kushiriki zoezi la usafi wa mazingira. “Zoezi la usafi wa mazingira katika korongo hili ni zoezi endelevu mpaka korongo letu litakapokuwa safi.
Mnapowaona viongozi wa halmashauri tupo nao hapa njue ni viongozi waliokuja kukagua usafi na kusimamia sheria. Hatua zikianza kuchukuliwa kwa wale ambao hawatekelezi maelekezo ya usafi wa mazingira mjue ni utekelezaji wa maelekezo rasmi kwa mujibu wa sheria” alisema Mogwa.