NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Arusha International Conference Center (AICC) Bw. Ephraim Mafuru amesema kuwa maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Rasilimali Watu unaotarajia kufanyika kuanzia Julai 25 hadi 26, 2023 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam umekamilika, huku akibainisha watanzania wanapaswa kutumia fursa hiyo ikiwemo kuongeza mapato kwa kutumia vyanzo vya utalii.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Bw. Mafuru, amesema kuwa vifaa vyote vinavyotarajia kutumika katika mkutano vimekamilika ili kuhakikisha kila kitu kinafanyika kwa ufanisi.
Bw. Mafuru amesema kuwa Tanzania ni nchi ambayo inapendwa na kukubalika Kimataifa katika kuwa mwenyeji wa Mikutano mikubwa.
“Tanzania inashika nafasi ya tano Bara la Afrika kuwa mwenyeji wa maandalizi ya mikutano yote inayofanyika Afrika ikiwa na asilimia 10” amesema Bw. Mafuru.
Amesema kuwa mpaka sasa kumbi zote zonazohusika na mkutano huu maandalizi yamekamilika ikiwemo vifaa vya kufanya tafsiri, kuimarisha ulinzi pamoja na kuwashwa taa zote za barabarani.
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka wananchi wa mkoa huo kukuza kipato na kuimarisha uchumi kupitia fursa zitakazopatikana kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu.
“Tutakuwa na wageni wasiopungua 1200, ambao watakula, watalala na watatembelea maeneo mbalimbali,” amesema Chalamila na kueleza kuwa wageni hao wanatarajia kuanza kuwasili Dar es Salaam Jumamosi Julai 22.
Amesema zaidi ya hoteli 40 zitatumika na wageni hao, hivyo mkutano huu pia ni fursa ya kutangaza utalii wa nchi na wamejiandaa kutangaza bidhaa zilizopo nchini kupitia mabanda ya wafanyabiashara.
“Ushiriki wa wafanyabiashara ambao tumewaleta hapa watakuwa zaidi ya 100 na wamekwisha andaliwa vizuri kuhusiana na bidhaa, aina ya bidhaa, uzzaji wao kwa ujumla pia kujali wateja ‘Customer Care’ na kujiunga na maandalizi haya hakuhitaji gharama zozote,” amesema Chalamila
Hata hivyo, Chalamila amesema mkutano huu ni matunda ya juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuifungua nchi na kuwa kiongozi wa kutangaza utalii wa nchi ikiwemo utalii wa mikutano hivyo fursa mbalimbali zinaendelea kufunguka nchini.