Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula ametekeleza ahadi yake ya ujenzi wa barabara za mitaa ya kata ya Shibula aliyoitoa kwa wananchi wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero na kuhamasisha maendeleo jimboni
Akizungumza wakati wa utekelezaji wa ahadi hiyo, Mratibu wa Mbunge sekta ya miundombinu Ndugu Mpunzi Mbegeje Kasubi amesema kuwa Mbunge Dkt Angeline Mabula ametenga kiasi cha shilingi milioni sita kutoka katika mfuko wake binafsi kwaajili ya kukodi greda litakalotumika kujenga barabara yenye urefu wa zaidi ya kilomita 10.1 ikijumuisha barabara ya kutoka Bogolanya kuelekea Igogwe Km 1, Igombe Saccos kuelekea Kisundi Km 3 na Butindo kuelekea Kilabela Km 4 na ya kutoka Shibula senta kuelekea Butindo
‘.. Mhe Dkt Mabula ameamua kutekeleza ahadi yake ya kuwajengea barabara, kikubwa tuendelee kumuunga mkono Mbunge wetu na Serikali ya Rais wetu Dkt Samia kwa kutuletea maendeleo ..’ Alisema
Aidha Ndugu Mpunzi amewapongeza wananchi wa kata ya Shibula kwa utayari wao na Wenyeviti wa Serikali za mitaa ya kata hiyo kwa ushirikiano wanaoutoa kwa ofisi ya Mbunge katika kutatua kero za wananchi
Leonard Moshi ni Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Shibula mbali na kumshukuru Mbunge Dkt Angeline Mabula Kwa kutekeleza ombi lao la ujenzi wa barabara korofi ndani ya kata Yao, amewapongeza wananchi wake Kwa kukubali kutoa maeneo yao yaliyopitiwa na barabara bila kudai fidia na posho
Canseline Samike ni mjasiriamali Mama Lishe ambae ameshukuru Kwa ujenzi wa barabara ya kutoka Shibula senta kuelekea Butindo kwani walikuwa wakipata changamoto ya kupanda kwa bidhaa kutokana na kero ya ukosefu wa usafiri wa uhakika pamoja na kupungua Kwa vifo vya mama wajawazito vilivyotokana na kujifungulia njiani Kwa kukosa usafiri wakati wa usiku pindi wanapozidiwa
Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula inaendelea na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo jimboni Kwa fedha za mfuko wa Jimbo, Serikali kuu, Mapato ya ndani ya halmashauri, Wadau wa maendeleo pamoja na fedha binafsi za mbunge wa Jimbo hilo