Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Albert Chalamila akizungumzia maandalizi ya mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika unaotarajiwa kufanyika Julai 25-26 mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano wa JNICC jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Ukimbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha AICC/JNICC Bw. Ephraim Mafuru akifafanua jambo katika mkutano huo uliofanyika Leo jijini Dar es alaam.
Balozi Mindi Kasiga Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kushoto akiwa na Upendo Gondwe kutoka kituo cha Uwekezaji TIC wakati mkutano huo ukiendelea.
(PICHA NA JOHN BUKUKU
……………………………….
Na Grace Semfuko, MAELEZO.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Albert Chalamila amewataka wakazi wa mkoa huo kuchangamkia fursa za kibiashara katika Mkutano Mkubwa wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusiana na ajenda ya rasilimali watu unaotarajia kufanyika Jijini Dar es Salaam Julai 25 na 26.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam leo Julai 21, Chalamila amesema ni muhimu wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuwapokea wageni watakaoingia katika Jiji hilo kutokana na kuwepo kwa fursa za kiuchumi kupitia fedha za kigeni.
Bw. Chalamila pia amewataka wakazi wa Mkoa huo kuupokea ugeni huo muhimu kwani ni fursa kiuchumi.
“Napenda kuwataarifu wakazi wenzangu wote wa Jiji la Dar es Salaam kwamba mikutano hii ni sehemu ya utalii, na ndio kitu hasa ambacho Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akikihamasisha, na ujio wa ugeni huu ni muhimu katika kujenga utalii wa mahoteli, utalii wa fukwe, utalii wa vyakula vya kitanzania, pamoja na utalii mwingine, kwa mantiki hiyo kutakuwa na wageni wasiopungua 1,200 ambao watakula, watalala na kutembelea maeneo mbalimbali” amesema B. Chalamila.
Amesema tangu mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani ameweza kuwekeza nguvu nyingi sana katika kubadili na kukuza taswira ya Nchi Kimataifa na faida zake sasa zimeshaanza kuonekana kwamba kupitia mkutano huo mkubwa ambao utafanyikia hapa kwetu Tanzania Tanzania imewekwa mwenye Ramani ya Dunia.
“Kwa hiyo nipende kuwapa taarifa hii wana Dar es Salaam wote kwamba ni muda sasa wa kutumia fursa hii kuweza kukuza mapato yetu na kukuza uchumi wa mkoa wa Dar es Salaam, ili wageni wa Dar es salaa waondoke wakiwa na picha nzuri ni muhimu nasi tukaonesha taswira nzuri katika kuwapokea wageni wote, lengo ni kuhakikisha kila mgeni anaefika katika mkoa wa Dar es Salaam anaacha Dola na na ndio maana tumehamasisha wajasiriamali mbalimbali kushiriki katika maonesho na kuuza bidhaa zao katika viwanja hivi ambavyo mkutano huu utakuwa unaendelea” amesema Bw. Chalamila.
Amezitaja sababu za Benki ya Dunia kuamua kufanya mkutano huo mkubwa na wa heshima Jijini Dar es Salaam kuwa ni pamoja na Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa amani ambapo ajenda muhimu ya rasilimali watu itakayojadiliwa ilihitaji nchi yenye utulivu na watu kusikilizana, suala la ajira kwa vijana ambapo azimio la Dar es Salaam litaziwezesha nchi hizo kujifunza kwa Tanzania kupitia mfumo wa vyuo vya VETA na vya ufundi mbalimbali Pamoja na miradi mikubwa inayoendelea ikiwepo ya SGR na mingine mingi.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Ukimbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha AICC/JNICC Bw. Ephraim Mafuru amesema wamejiandaa vizuri katika kuupokea na kuuhudumia ugeni huo wa Wakuu wa Nchi za Afrika.