Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM Taifa, Ndg. Sophia Mjema, leo tarehe 20/7/2023 ameitembelea Kampuni ya Africa Media Group Limited inayomiliki Channel 10, Channel 10 Plus, Magic FM Redio na Classic FM Redio katika muendelezo wa ziara yake ya kuvitembelea vyombo vya habari vya hapa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Africa Media Group Limited Ndg. Shabani Kissu alimkaribisha Mwenezi Mjema kwa niaba ya wafanyakazi, ambapo alitembelea ofisi na studio za televisheni na redio, na kujionea shughuli zinazofanywa na vituo hivyo.
Akiwa katika studio za Magic FM Redio Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM Ndg. Sophia Mjema alijibu swali kuhusu uwekezaji na uendelezaji wa bandari, ambapo aliwataka Watanzania waelewe ni utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kuimarisha uchumi, kwa kuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato, hivyo wasiwe na hofu na waulize maswali na kutoa maoni na Serikali ya CCM ni sikivu itayafanyia kazi.
Akisisitiza kuhusu uwekezaji wa bandari Mjema, ameviomba vyombo vya habari kuandika kwa usahihi kile Serikali inachokifanya ambacho ni dhamira ya dhati ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha uchumi wa Taifa.
Aidha, ametoa wito kwa Watanzania kumuunga mkono Rais katika dhamira yake ya dhati ya kuwaletea maendeleo.