Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasalimia wananchi wa Makambako mkoani Njombe wakati akiwa safarini kuelekea mkoani Ruvuma kwaajili ya ziara ya kikazi. Tarehe 20 Julai 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na wananchi wa Makambako mkoani Njombe wakati akiwa safarini kuelekea mkoani Ruvuma kwaajili ya ziara ya kikazi. Tarehe 20 Julai 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Makambako mkoani Njombe Deo Sanga akieleza mafanikio na changamoto mbalimbali za jimbo hilo wakati Makamu wa Rais aliposimama katika eneo hilo akiwa safarini kuelekea mkoani Ruvuma kwaajili ya ziara ya kikazi. Tarehe 20 Julai 2023.
……
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewaasa wananchi wa mkoa wa Njombe pamoja na wakulima kwa ujumla kuacha tabia ya kuuza zao la parachichi kabla hazijakomaa kwani kwa kufanya hivyo kuna athiri soko la zao hilo kimataifa.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 20 Julai 2023 wakati akizungumza na wananchi wa Makambako mkoani Njombe akiwa njiani kuelekea mkoani Ruvuma kwaajili ya ziara ya kikazi. Ameitaka Wizara ya Kilimo kusimamia vema taratibu za uuzaji wa mazao ili kuweza kulinda soko la mazao ya Tanzania pamoja na kuwa endelevu. Pia ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Njombe kuhakikisha unatoa elimu kwa wananchi juu ya hasara zinazopatikana kutokana na kuuza zao hilo likiwa bado halijakomaa.
Halikadhalika Makamu wa Rais ameigiza Wizara ya Kilimo kufanya tathimini ya mahitaji ya pembejeo hususani katika mikoa inayozalisha mazao ya chakula kwa wingi. Aidha amesema ni muhimu kuongeza juhudi katika kuhakikisha vipimo sahihi vinatumika wakati wa kuuza mazao ili kuwawezesha wakulima kupata haki ya mazao waliozalisha.
Makamu wa Rais amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Njombe kwa utunzaji wa mazingira na kuwaasa kuepukana na tabia za uchomaji moto unaoleta athari katika misitu.
Aidha Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa mkoa huo hususani wanawake kujiunga katika vikundi ili kuanza utaratibu wa kutengeza mkaa unaotokana na makaa ya mawe yanayopatikana mkoani humo na hivyo kushiriki katika jitihada za kulinda mazingira.
Vilevile amewataka wananchi wa mkoa wa Njombe kuhakikisha wanasimamia suala la watoto wao kupata elimu pamoja na kuzingatia lishe kwa watoto hao ili kuwa na mustakbali mzuri kwa taifa sasa na baadae. Pia amewasihi wananchi wa mkoa huo kuendelea na jitihada za kujikinga na ugonjwa wa UKIMWI.