Muwakilishi wa Naibu Waziri Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Leah Kihimbi afungua mafunzo ya wajumbe wa Kampuni ya Kukusanya na Kugawa Mirabaha (CMO) kwa kazi ya Muziki iitwayo Tanzania Music Rights Society (TAMRISO) itakayopewa Leseni .
Mafunzo hayo yamefanyika leo Julai 20, 2023 Jijini Dar es Salaam na yameandaliwa na COSOTA kwa kushirikiana na Shirika la Miliki Bunifu Duniani (ARIPO) .
Lengo la mafunzo hayo ilikuwa ni kuwajengea uwezo viongozi wa TAMRISO na wadau wa Muziki wa namna ya kusimamia na kuziendesha CMO pamoja na kueleza wajibu wa TAMRISO kwa wanachama wake.
Akizungumza katika mafunzo hayo Muwakilishi huyo wa Naibu Waziri alisisitiza viongozi TAMRISO kufanya kazi zao kwa weledi na kwa uwazi ili kuondoa migogoro, vilevile aliwasihi Wasanii wa Muziki kujiunga na kampuni hiyo ili kuweza kunufaika na matumizi ya kazi zao.
“Serikali imetekeleza ombi lenu la muda mrefu la kuanzisha kampuni za kukusanya na kugawa mirabaha nitoe rai kwenu mkafanye majukumu vizuri ni matarajio yetu hivi sasa mtanufaika zaidi, pia natoa pongezi kwenu kwa kuwa kupata Leseni hii,” alisema Leah.
Nae Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Miliki Bunifu la Kikanda la Afrika (ARIPO) Amadu Bah alipongeza COSOTA kwa jitihada walizozifanya na kukamilisha kuanzishwa kwa CMO nchini baada ya mabadiliko ya sheria ya mwaka 2022.
“ARIPO tupo tayari kushirikiana na TAMRISO kama CMO mpya ya nchini Tanzania na tutaendelea kuwapa mafunzo mbalimbali ili kuweza kuwaimarisha,” alisema Bah.
Kwa upande wa Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki COSOTA Doreen Anthony Sinare amesema tutaendelea kutoa kutoa ushirikiano kwenu TAMRISO kwa kuwashauri wakati wote.