Na Dotto Mwaibale, Singida
MBUNGE wa Singida mjini, Musa Sima amesema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan
amefanya kazi kubwa mno na amewaomba watanzania kumuombea ili Mungu aendelee
kumpa afya njema na maisha marefu yenye baraka na fanaka katika kuliongoza
Taifa letu.
Sima ameyasema hayo Julai 18, 2023 wakati akihutubia wananchi wa Kata ya
Unyianga iliyopo Manispaa ya Singida katika mkutano wa hadhara alioufanya baada
ya kutembelea miradi ya maendeleo na kuikagua katika muendelezo wa ziara yake
alioianza juzi jimboni humo.
Alisema Rais Samia amekuwa akifanya kazi kubwa na ngumu yenye uadilifu
hivyo kila mpenda maendeleo hapa nchini anapaswa kumpongeza na kumuombea.
“Mimi na wenzangu wa maeneo mengine ambao tumenufaika na uongozi wake
katika awamu yake hii ya sita tunakilasababu ya kumtolea salamu za kumshukuru
mbele yenu yeye hawezi kufika hapa na tulipokuwa tunazungumzia mafiga matatu
tunaanza na la kwake, mbunge na diwani,” alisema Sima.
Alisema kazi katika nchi hii imefanyika kubwa na kuwa Rais Samia sio
msemaji sana kama walivyo wanawake wengine wao ni watendaji wakuu na watu wenye
huruma kwani wakisema bungeni anawasikiliza na wanapoizungumzia Singida imepata
miradi mikubwa na yenye fedha nyingi sana.
“Ndugu zangu tumepata miradi ya maji, umeme, barabara, afya na kila
kitu, nilipokuja mara ya kwanza hapa changamoto kubwa ilikuwa ni maji na sio
hapa tu bali ilikuwa karibu maeneo mbalimbali ya jimbo la Singida mjini na hela
tuliyokuwa tukiipata ilikuwa ndogo bilioni 2 au 3 na kuigawanya kwenye maeneo
yote ilikuwa ni changamoto lakini umetokea mradi wa maji wa miji 28 kwa nchi
nzima na moja ya miji hiyo ilionufaika ni Manispaa ya Singida ambapo tupewa Sh.Bilioni 40
jambo ambalo litaweza kurudi bungeni na kuomba fedha za maji nitachekwa,”
alisema Sima huku akishangiliwa na wananchi.
Alisema kupitia mradi huo wananchi wajue wanakwenda kusahau kabisa kama
walikuwa na changamoto ya maji ndani ya Manispaa ya Singida kwani watayatumia
na kubaki na ziada kubwa hivyo wamshuruku Rais Samia kwa kutoa fedha hizo
ambazo tayari zipo kwa wataalam na kazi hiyo ya ujenzi imeanza ambapo hadi
kukamilika itachukua miezi 12 hadi 24 kwa jimbo zima na akawaomba wananchi
kutoa ushirikiano kwa wafanyakazi wa mradi huo pamoja na kuitunza miundombinu.
Sima alisema yeye tangu awe mbunge fedha alizopata kwa ajili ya kutekeleza
miradi katika jimbo lake ni nyingi mno achilia mbali majimbo mengine nchini
kote sasa inakuwaje watu wasema hakuna kazi iliyofanyika chini ya uongozi wa
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Mbunge Sima akizungumzia kazi nyingine kubwa aliyoifanya Rais Samia Suluhu
Hassan ni kupokea maombi yake ya kuomba majengo ya iliyokuwa Hospitali ya Mkoa
wa Singida yatumike kuwa Hospitali ya Wilaya (Hospitali ya Manispaa
Singida) ili wananchi waendelee kupata
huduma karibu na gharama zake zitakuwa nafuu kwa wale ambao watakuwa hawana
bima.
Alisema kama haitoshi wamejenga vituo vya afya viwili, Unyambwa, Mwaja na
bado kwa kupitia mapato ya ndani wameshirikiana na madiwani wamejenga kituo cha
afya Kata ya Mtipa na sasa wanakamilisha Zahanati katika Kata hiyo ya Unyianga
ambayo ilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi na Serikali ikawapa sapoti.
Mbunge Sima akiendelea kuzungumzia uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam
alisema haijauzwa isipokuwa wananchi wanachanganywa kutokana na jambo hilo kuwa
na maneno mengi kutoka kila pande.
Alisema wananchi wanapaswa kuwauliza wabunge kile walichokiridhia na
kukipitisha badala ya kuyumbishwa na maneno ya watu ambayo hayana tija katika
uwekezaji huo mkubwa wenye manufaa kwa Taifa.
Alisema katika nchi hii uwekezaji haujaanza leo na fedha nyingi za miradi
inayotekelezwa zinatokana na uwekezaji na ndani ya Manispaa ya Singida akianza
kujumulisha miradi ya elimu, afya na barabara hazipungui bilioni 10
akichanganya na bilioni 41 za mradi wa maji, Tanroads, Tarura, umeme zinaweza
kukaribia kufika hadi Sh. Trilioni moja katika kipindi cha muda mfupi alichokaa
madarakani Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kwanini nisitumie fursa yangu kumuombea mama huyu kwa Mungu ili
aendelee kuliongoza Taifa ili kwa maana tunapata fedha nyingi sana,”
alihoji Mbunge Sima huku akishangiliwa na wananchi.
Sima alisema fedha zote hizo zinakuja kutokana na uwekezaji hasa
panapokuwepo na Rais mwenye maono ambaye anawajali wananchi wake kwa
kuhakikisha huduma za jamii zinapatikana.
Alisema leo anakuja mwekezaji lakini wakati huohuo kuna watu wanaibuka
kufanya upotoshaji ili kukwamisha uwekezaji huo watu hao hawaitakii mema nchi
yetu na wana lengo la kuwagawa watanzania.
Alisema wabunge wanaowajibu wa kuridhia makubaliano ya mkataba kati ya
Tanzania na nchi nyingine kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ibara ya 63 tatu.
Alisema wakiwa wawakilishi wa wananchi walichokiridhia ni sahihi hakuna
eneo waliloridhia kwa ajili ya kuliangamiza taifa la Tanzania.
Awali kabla ya Mbunge Sima hajazungumza na wananchi katika mkutano wa
hadhara Diwani wa Kata hiyo, Geofrey Mdama alipata fursa ya kuelezea miradi
mbalimbali ya maendeleo iliyofanyika baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa
fedha nyingi ambapo naye alitumia nafasi hiyo kumpongeza.
Mbunge Sima akiwa akiwa katika ziara hiyo aliongozana na wajumbe wa kamati
ya Siasa ya Wilaya ya Singida ambapo alitembelea Shule ya Sekondari ya Unyianga
na kuzungumza na wanafunzi pamoja na walimu kabla ya kweda kukagua ujenzi wa
Zahanati ya Unyianga.
Katika ziara hizo za Mbunge Sima wananchi wamekuwa wakionesha imani kwake kutokana
na jinsi ambavyo anawatumikia na kufikia hatua ya kushindwa kuvumilia na
kuonesha upendo wao wa dhahiri kwake huku wakimshukuru kwa ushirikiano anaowapa
na kujitoa kuwasadia katika shughuli mbalimbali ambapo amekuwa akizawadiwa
zawadi na kufanyiwa dua.
Katika mkutano huo wananchi walimpa zawadi ya kuku na mbuzi pamoja na
diwani wa kata hiyo Geofrey Mdama ambapo pia wanawake 10 kutoka vyama vingine wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata hiyo Elizabeth Benedict ambao wamejiunga na CCM kufuatia kuridhishwa na kazi nzuri za maendeleo zinazofanywa na Rais Samia,Mbunge wao Musa Sima na Diwani Geofrey Mdama.
Kesho Mbunge Sima anatarajia kuendelea za ziara yake kwa kutembelea na kukagua miradi
mbalimbali ya maendeleo katika Kata ya Kisaki na kuzungumza na wananchi kwenye
mkutano wa hadhara akiongozwa na diwani wa kata hiyo, Moses Ikaku.