Na Shamimu Nyaki
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amepongeza juhudi za mdau wa michezo Kuambiana Investment kwa kuanzisha mashindano ya Kuambiana Cup katika Wilaya ya Ludewa ambayo yanasaidia kuibua vipaji, kukuza na kuendeleza
michezo.
Mhe. Chana ametoa pongezi hizo Julai 18, 2023 Ngelenge Manda wilayani hapo wakati akifungua mashindano hayo yaliyoandaliwa na mdau wa Michezo Bw. Imani Kuambiana, ambapo amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inaweka mazingira mazuri kwa wawekezaji kukuza michezo kuanzia ngazi ya kijiji.
“Wizara kwa mwaka huu wa fedha inaanza Ukarabati wa Viwanja kwa majiji Saba ikiwemo Mwanza, Tanga, Arusha na Mbeya , pamoja na Shule mbili katika kila mkoa ambazo idadi yake ni 56, na tayari tumeanza kuboresha Chuo chetu cha Malya ambacho kinazalisha Wataalam wengi zaidi” amesema Mhe. Chana.
Ameongeza kuwa, Sekta ya Utamaduni na Sanaa inasaidia kuunganisha jamii na kutoa fursa ya ajira kwa watanzania, huku akisistiza kuwa, Tamasha la pili la Utamaduni litakalofanyika mwezi ujao Mkoani Njombe, litatoa fursa kwa vikundi vya Utamaduni na Sanaa kuonesha vipaji na kutangaza Mila na desturi za mikoa yao.
Kwa upande wake muandaji wa Mashindano hayo Bw. Imani Kuambiana amesema lengo la mashindano hayo ni kutoa nafasi kwa vijana waliopo wilayani hapo kuonesha uwezo wao ambapo amealika wadau wengine kuja kuona vipaji hivyo na kuviendeleza.
Mashindano hayo yamejumuisha Tarafa tatu za Wilaya hiyo na Mshindi atapata Kombe na wengine watapata Jezi pamoja na pesa taslim.