Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mgeni wake Rais wa Hungary Mhe. Katalin Novák waliwasili katika viwanja vya Ikulu ili kuzungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Julai, 2023. Rais Novák yupo nchini Tanzania kwa ziara ya siku tatu.
(PICHA NA JOHN BUKUKU)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mgeni wake Rais wa Hungary Mhe. Katalin Novák wakiwasili katika viwanja vya Ikulu ili kushuhudia itiaji saini wa makubaliano ya Ushirikiano na kuzungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Julai, 2023. Rais Novák yupo nchini Tanzania kwa ziara ya siku tatu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mgeni wake Rais wa Hungary Mhe. Katalin Novák wakishuhudia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolph Mkenda pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kutoka Hungary Tristan Azbej aliyeiwakilisha Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Nchi hiyo wakati wakisaini Hati ya Makubaliano baina ya nchi mbili kuhusu Ushirikiano wa ndani wa Programu ya Stipendium Hingaricum ya mwaka 2024-2026, Ikulu Jijini Dar es Salaam. Stipendium Hingaricum ni Programu ya ufadhili wa masomo ya Elimu ya Juu (Scholarship) inayotolewa na Serikali ya Hungary kwa ajili ya Wanafunzi wa kigeni.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolph Mkenda pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kutoka Hungary Tristan Azbej aliyeiwakilisha Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Nchi wakisaini Hati ya Makubaliano baina ya nchi mbili kuhusu Ushirikiano wa ndani wa Programu ya Stipendium Hingaricum ya mwaka 2024-2026, Ikulu Jijini Dar es Salaam. Stipendium Hingaricum ni Programu ya ufadhili wa masomo ya Elimu ya Juu (Scholarship) inayotolewa na Serikali ya Hungary kwa ajili ya Wanafunzi wa Kigeni.
Rais wa Jamhuri ya Muumgano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waandishi wa Habari Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Julai, 2023.
Rais wa Hungary Mhe. Katalin Novák akizungumza na Waandishi wa Habari Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Julai, 2023.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Waziri wa Elimu , Sayansi na Tekonoloji Profesa Adolf Mkemda kushoto na Prof. Kitila Mkumbo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ikulu Leo.
Na Mwandishi wetu
NCHI ya Tanzania na Hungary zimeingia makubaliano ya kushirikiana katika maeneo mbalimbali huku kipaumbele kikiwa katika kuendelea kubadilishana wanafunzi wa elimu ya juu hasa katika eneo la sayansi, tekonolojia, uhandisi na hisabati.
Makubaliano hayo yametangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa upande na Tanzania na Rais Katalin Novak wa Hungary wakati wakizungumza na waandishi wa habari Leo Julai 18, 2023 Ikulu Dar es Salaam.
Rais Katalin yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo aliwasaili Julai 17 na anatarajiwa kuondoka Julai 20 mwaka huu, ambapo leo atakuwa katika safari binafsi huko jijini Arusha.
Akizungumzia ziara hiyo Rais Samia amesema Tanzania na Hungary zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu katika eneo la elimu uwekezaji na biashara, hivyo utiaji saini uliofanyika kati ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania Profesa Adolf Mkenda na Waziri wa Mambo ya Nje wa Hungary Tristan Azbej unaenda kufungua ukurasa mpya kwa nchi hizo kwenye sekta husika.
Amesema kwa miaka mingi nchi hiyo imekuwa ikifadhili wanafunzi wa Tanzania kwenda masomo katika ngazi ya shahada ya kwanza, uzamili na uzamivu, hivyo katika kuhakikisha wanaunga mkono juhudi hizo Tanzania itakuwa inatoa ufadhili kwa wanafunzi 30 kutoka Hungary kuja kusoma masomo ya elimu ya juu.
“Pia tumekubaliana umuhimu wa kuanzisha mashauriano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Hungary. Hii itawezesha Serikali zetu kushirikiana na kufanya mashauriano juu ya maeneo yenye maslahi ya pamoja tuliyokubaliana,” alisema Rais Samia.
Mkuu huyo wa nchi amesema katika mazungumzo yao wamekubaliana kushirikiana kuhamasisha wawekezaji katika sekta ya utalii ambayo imeonesha kukua kwa kasi.
Amesema kwa takwimu za hivi karibuni zaidi ya watalii 70,000 wametembelea Tanzania, hivyo kumuomba Rais Katalin kuwa balozi mzuri katika kuvitangaza vivutio vya utalii.
“Tanzania ina vivutio vingi vya utalii, tunakuomba Mheshimiwa Rais Katalin ukirudi nyumbani uwe balozi wetu, lakini pia ili kufanikisha majadiliano na makubaliano yetu tuangalie nanma ya kuwa na ushirikiano wa kidiplomasia,” alisema.
Rais Samia ametaja eneo lingine ambalo wamejadiliana na Rais Katalin ni kuhusu usawa wa kijinisia na uwezeshwaji wanawake ambapo matarajio yao ni kuhakikisha mwanamke anainuka kiuongozi.
Kwa upande wake Rais Katalin amesema wameingia makubaliano ya kushirikiana katika eneo la elimu kwa kuwa elimu ndio kipaumbele kwa kila upande na kwamba wataendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 200 ambao watataka kusoma nchini Hungary.
Katalin amesema Tanzania ikiwa ni moja ya nchi ambayo idadi ya watu inaongezeka kwa kasi ni muhimu kuweka mkazo katika elimu ili kuweza kutatua changamoto zake.
“Katika eneo la usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi, hapa tunataka kuweka mkazo kwa kuwa wanawake wengi wapo nyuma katika kushiriki siasa na uongozi. Tunapaswa kuwekeza kwa wasichana ili waweze kushiriki uongozi na wafikie huku tulipo fikia mimi na Rais Samia,” alisema.
Amesema iwapo mataifa haya mawili yatashirikiana kwa kila sekta ni wazi kuwa maendeleo yatapatikana kwa haraka.
Aidha, amemualika Rais Samia kushiriki mkutano wa viongozi wanawake ambao nchi ya Hungary itaandaa mwakani, ili waweze kujadiliana namna ya kukomboa kundi hilo kisiasa, kiuchumi na kijamii.