Na. WAF, Njombe
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe ameupongeza Uongozi na watumishi wa Mkoa wa Njombe kwa kutoa Huduma zinazokubalika na wananchi ambazo ni moja ya kiashiria cha utoaji wa Huduma bora za afya.
Dkt. Magembe amebainisha hayo leo Mkoani Njombe katika ziara yake ya kikazi ambapo ametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, Hospitali ya Wilaya ya Makete na Hospitali ya Kibena na kujionea hali ya utoaji Huduma za afya katika Hospitali hiyo.
Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu alipata nafasi ya kufanya mahojiano na baadhi ya wagonjwa na ndugu zao ili kupata mrejesho wa utoaji wa huduma katika vituo hivyo vya serikali.
“Kwa kweli tangu nimekuja hapa nimepewa huduma nzuri sana, vipimo, dawa na hata usiku tuko na wahudumu humu wodini wantuhudumia bila kuchoka. Hospitali yetu ya Mkoa ina vifaa vya kisasa, tulikuwa hatujawahi kuona CT-scan sasa ipo, tunamshukuru sana Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kutuboreshea huduma na kutupunguzia mwendo kwenda Mbeya” aliongea mmoja wa wagonjwa aliyelezwa wodi ya upasuaji ya wanaume
Dkt. Magembe ameutaka mkoa huo kuendelea kufanya ukaguzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi na kufanya ukaguzi wa ubora wa Huduma kila robo mwaka ili kubaini mapungufu na kuyafanyia kazi haraka na pia kuendeleza mambo mazuri.
Amewasisitizia watumishi kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu, weledi na maadili ya viapo vya taaluma zao ili wananchi waendelee kuwa na imani na kuzitumia huduma za afya ambazo kwa sasa zimeboreshwa sana.
“Mkoa wa Njombe bado kuna changamoto ya lishe duni hasa kwa watoto ikiwemo udumavu ambao ni takribani asilimia 50. Mkoa wa Njombe unavyo vyakula vingi vya kutosha, hivyo maafisa lishe na watumishi wote tujikite kutoa elimu kwa wananchi namna ya kuandaa, kutunza na kuwalisha watoto kwa kutumia vyakula vilivyoko kwenye mazingira yao”,ameeleza Dkt Grace
Amewataka pia kusimamia kikamilifu swala la utoaji chanjo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na kutoa elimu kwa wasichana kupata dozi kamili ya chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi.
Nae Katibu Tawala wa Mkoa Bi Judica Omari amewahakikishia Manaibu Katibu Wakuu Afya na TAMISEMI kuwa wataendelea kutekeleza mikakati na maelekezo ya serikali ili kuhakikisha afya za wanachi wa Njombe zinaimarika.
Aidha, amemshukuru Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika ndani ya Mkoa wa Njombe ikiwemo afya ndani ya kipindi kifupi sana.