Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewatoa hofu watanzania kuwa nchi ipo sehemu salama kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suruhu Hassani kwa kushirikiana na watendaji mbalimbali wanaendelea kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM.
Akizungumza leo tarehe 16/7/2023 katika Mkutano Mkoani Mtwara, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Daniel Chongolo, amesema kuwa kiongozi mkubwa wa nchi anaendelea kuwatumikia watanzania kwa kupanga majeshi na kuratibu mipango ili kufikia malengo tarajiwa.
“Hatuna hofu, mashaka na tutaendelea kutekeleza kutokana na ilani ya chama cha mapinduzi na wanaohangaika kuongea wamekosa muda na muelekeo” amesema Ndugu Chongolo.
Ndugu Chongolo amesema kuwa Rais Dkt. Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) amekuwa akiongoza njia pamoja wana CCM kuzingatia ilani.
“Kuna watu wanaongea kama kwamba Rais kila kitu anafanya yeye, hao watu ni wachonganishi, wazushi, wanatengeneza mazingira ya kuwagombanisha wana CCM na viongozi wenu” amesema Ndugu Chongolo.
Ameeleza kuwa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ina kurasa 303 ndiyo imebainisha utekelezaji wa miradi ya barabara katika Mkoa wa Mtwara.
“Tunapotekeleza miradi mbalimbali hawasemi kwa nini tunajenga kwa sababu wanajua tukiendelea kutekeleza kwa ufanisi kazi yao itakuwa ngumu huku mbele” amesema Ndugu Chongolo.
Amefafanua kuwa ukichukua ilani ya uchaguzi wa chama cha mapinduzi ibara ya 22 imeeleza namna ya mipango ya uwekezaji ikiwemo katika bandari.
Amesema kuwa pia ibara ya 59 ukarasa wa 92 imeweka wazi kwa kubainisha namna ya mipango ilivyowekwa na ilivyo katika bandari zote nchini.
“Tayari tumewangundua baadhi ya watu njia wanazotumia ndiyo maana tunaitwa chama tawala nchini kwani kuongoza nchi ni kazi ambayo inaitaji kuwa makini” amesema Ndugu Chongolo.
Ameeleza kuwa “Ukimuona adui yako anakupigia makofi unapofanya jambo achana nalo kimbia na tengeneza mkakati mipya wa kulitenda, ukiona amenuna anahangaika, anapambana lisifanikiwe, kanyaga mwendo kwani hilo ndiyo jambo sahihi” amesema Ndugu Chongolo.