NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuboresha utendaji wa bandari zote za Tanzania kwa kuzingatia maelekezo ya ilani ya Chama.
Akizungumza leo tarehe 15/7/2023 Jijini Mbeya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Daniel Chongolo, amesema kuwa miradi yote inayotekelezwa na serikali imetokana na misingi ya Chama kwa kile wanachokiamini ili kuleta tija kwa maendeleo ya Taifa.
Ndugu Chongolo amesema kuwa CCM wamekuwa makini katika utekelezaji wa ilani kwa kuzingatia ahadi ambazo wamekuwa wakitoa ikiwemo ujenzi wa barabara.
“Bandari zote zitafanyiwa maboresho ikiwemo ya mkoa wa Tanga, Mtwara pamoja Dar es Salaam kutokana na kwamna hilo lipo katika ilani ya CCM” amesema Ndugu Chongolo.
Amesema kuwa CCM ina malengo na mipango katika kuhakikisha wanapiga hatua katika kuwaletea maendeleo watanzania.
“Ilani ya CCM imebeba matumaini ya utatuzi wa changamoto za wananchi katika kila nyanja” amesema Ndugu Chongolo.
Hata hivyo Ndugu Chongolo ameitaka serikali kuendelea na mchakato wa awamu ya pili katika makubaliano ya uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam.
Kwa upande wake Spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt. Tulia Ackson, amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 serikali imeweka bajeti ya trilioni 44.3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi.
Dkt. Ackson amebainisha kuwa ili kupata fedha watanzania wanapaswa kuonesha umoja na ushirikiano kwa kulipa kodi pamoja na kutafuta wawekezaji kwa ajili ya kufanikisha miradi ya maendeleo.
“Ili kupata fedha lazima tulipe kodi lakini wakati huo huo tutafute wawekezaji ili kakamilisha miradi ya maendeleo na malengo tuliyojiwekea , Bunge pia linaendelea kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kufikia lengo la utekelezaji wa bajeti” amesema Dkt. Ackson.