Na. Jacob Kasiri – Katavi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, CP Benedict Wakulyamba amelisisitiza Jeshi la Uhifadhi, Wanyamapori na Misitu kulinda Maliasili za nchi ili kuwavutia watalii wengi zaidi wanaotembelea nchini na kuliwezesha taifa kupata mapato mengi yanayotokana na utalii kwa Maendeleo ya nchi.
Aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Hifadhi ya Taifa Katavi iliyopo mkoani Katavi. CP Wakulyamba alisema
“Jukumu la Jeshi hili ni kulinda maliasili ili kuvutia watalii wengi zaidi na kukuza pato la taifa, na jukumu hili tumepewa kisheria hivyo ni wajibu wa kila mmoja kutekeleza kazi hizo kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.”
Hata hivyo, CP Wakulyamba alizitaka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuongeza ushirikiano tofauti na ilivyo sasa. Katika kuthibitisha hilo alisema, “inaonekana hakuna ushirikiano wa kutosha baina yenu, hivyo ni lazima mshirikiane ili muwe na umoja thabiti maana ulinzi wa maliasili unahitaji nguvu ya pamoja. Pia shirikianeni na majeshi mengine kama vile Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Polisi, Uhamiaji na Magereza kwa sababu kazi zenu zinategemeana”.
Naye, Naibu Kamishna wa Uhifadhi TANAPA Steria Ndaga, Mkuu wa Kanda ya Kusini alimpongeza CP Wakulyamba kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii na kumuaidi kumpa ushirikiano pamoja na kutekeleza maagizo yote aliyoyatoa.
Pia, Kamishna Ndaga alimshukuru CP Wakulyamba kwa ziara ya kikazi katika Hifadhi ya Taifa Katavi inayosifika kwa kuwa na viboko wengi, pia alielezea mafanikio yanayoendelea kuonekana baada ya Uzinduzi wa Filamu maarufu duniani ya “Tanzania Royal Tour” iliyoasisiwa na Mhe. Rais Samia
CP Wakulyamba alifanya kikao na Maafisa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi kutoka TAWA na TFS.