Afisa Vijana Mkoa wa Singida Frederick Ndahani (wa pili kushoto) akiwa na wajumbe wa Kamati ya Lishe wa Shule ya Msingi Nkalankala na Shule ya Sekondari ya Set Benjamin wakati akikagua chakula kilichopatikana kwa ajili ya wanafunzi wa shule hizo.
Na Mwandishi Wetu, Singida
AFISA Vijana Mkoa wa Singida Frederick Ndahani ameupongeza Uongozi wa
Shule ya Msingi Nkalankala na Shule ya Sekondari ya Set Benjamin pamoja na
wazazi wa Kata ya Nkalankala kwa kuamua
kutoa chakula kwa wanafunzi shuleni.
Ndahani ameyasema hayo wakati akifuatilia
Ufundishaji na hali ya utoaji wa chakula shuleni katika Shule za Msingi na
Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida.
Ndahani amewapongeza wazazi waliounda kamati ya
Lishe ya shule na kusimamia ,utoaji wa elimu ya umuhumu wa chakula,ukusanyaji,utunzaji
na upishi ambapo hadi sasa Shule ya Msingi Nkalankala imekusanya jumla ya
magunia 90 ya Mahindi, maharage gunia 20 na mafuta ya chakula lita 350 na Shule
ya Sekondari Set Benjamin tayari imekusanya magunia 33 ya mahindi,maharage gunia
12 ,mafuta ya chakula lita 150 na sukari kilogramu 25 hatua ambayo imesaidia
wanafunzi wote katika shule hizo kupata chakula shuleni.
Nawashauri viongozi na wazazi kuiga mfano wa
wazazi wa Nkalankala katika utoaji wa chakula shuleni na tukiamua tunaweza kuleta
mapinduzi ya elimu mkoani Singida kwa sababu watoto sasa watapata chakula na
kuwa watulivu darasani.
Kwa upende wake Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe
katika Shule ya Sekondari Set Benjamin Abduli Silimu amesema wazazi baada ya
kushirikishwa jambo hilo la uchangiaji wa chakula wamekubali kutoa chakula cha kutosha ambacho kitatumika
hadi msimu ujao wa chakula wa Juni 2024.
Katibu wa Kamati ya Lishe katika Shule ya Msingi
Nkalankala, Elizabeth Yona amesema
wajibu wa wazazi ni kutoa huduma bora kwa watoto.
” Serikali ina wajibu wake, walimu na Sisi
wazazi tunaowajibu wetu na moja ya wajibu ni kuwapatia chakula wanafunzi wakiwa
shuleni na nje ya shule,” alisema Yona.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Set Benjamin
Jackiline Molel na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nkalankala iliyopo Mkalama
wamesema wataendelea kusimamia utoaji wa Chakula Shuleni Kwa kushirikiana na
Wazazi wa Kata ya Nkalankala.