Mwandishi wetu, Simiyu
TAASISI YA uhifadhi ya Friedkin Conservation Fund (FCF) kwa kushirikiana na Kampuni ya Utalii ya Mwiba Holdings LTD wamezindua mradi wa kutoa chakula cha bure cha mchana kwa wanafunzi 856 wa shule ya Msingi Makao, wilayani Meatu mkoa wa Simiyu.
Mradi huo umezinduliwa na Mkuu wa wilaya ya Meatu, Fauzia Ngatumbura ambapo kampuni hizo zitakiwa zikitumika kiasi cha shilingi milioni 20.5 Kila mwezi kwa ajili ya kutoa chakula hicho cha mchana.
Mbali na chakula hicho,Taasisi hizo za uhifadhi,pia zimejenga jiko la kisasa kwa ajili ya shule hiyo ambalo limegharimu kiasi Cha shilingi milioni 28.1. na mradi wa uvunaji Maji ya mvua uliogharimu shilingi milioni 30.8.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa miradi hiyo, Mkuu huyo wa wilaya alipongeza Taasisi ya Friedkin na Mwiba Holdings kwa kutoa msaada huo mkubwa kwa wilaya ya Meatu ambao unaendana na Maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe bora.
Ngatumbura alisema mradi huo utasaidia kuongeza ufaulu wa wanafunzi ,kuondoa utoro lakini pia kuwapa Utulivu wanafunzi wakiwa darasani.
“Tunawashuru Friedkin na Mwiba na mradi huu ni utekelezwaji wa maagizo ya serikali kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula cha mchana mashuleni na naomba wawekezaji wengine katika wilaya hii waige miradi hii lakini pia wananchi maeneo mengine wajitokeze kuchangia chakula”alisema
Wakizungumzia mradi huo,Meneja wa miradi ya Maendeleo ya Jamii wa Friedkin Tanzania, Aurelia Mtui na Meneja miradi Maendeleo ya Jamii wa Friedkin Wilayani Meatu, Sylvester Bwasama walieleza mradi huo ni sehemu ya miradi inayofanywa kwenye Jamii zinazozunguka maeneo ya vijiji zaidi ya 25 katika wilaya hiyo waliowekeza shughuli za uhifadhi na Utalii.
“Tunaimani kubwa mradi huu utakuwa na matokeo mazuri na ni mradi endelevu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu Bora bila kuwa na changamoto nyingine”alisema Mtui.
Bwasama alisema licha ya mradi huo pia wanamradi wa ukamilishaji nyumba ya walimu na madarasa mawili katika shule ya msingi Mwajimoso iliyopo Kijiji cha Mwambagimu.
Pia tumejenga mfumo wa uvunaji Maji ya mvua shule ya sekondari Makao,tunawezesha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi na vijana kuelewa umuhimu wa Utalii na uhifadhi.
“Pia tunasaidia miradi ya ufugaji nyuki na vikundi vya COCOBA na VICOBA, tunasaidia Kukabiliana na Wanyama wakali na waharibifu katika maeneo ya hifadhi kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori(TAWIRI) na Mamlaka ya Usimamizi wanyamapori (TAWA)kuwafungiwa Tembo mikanda ya kielekroniki ya kusoma mawimbi”alisema
Lakini pia tumejenga nyumba ya Askari wa wanyamapori kukabiliana na ujangili na Kudhibiti wanyamapori waharibifu.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Meatu, Anthony Philipo alisema miradi hiyo iliyozinduliwa inatoka na ushirikiano mzuri uliopo sasa baina ya mwekezaji katika eneo la Ranchi ya Mwiba na Makao WMA.
“Sisi tunaushirikiano mzuri sana na Mwekezaji huyu Mwiba na amekuwa akisaidia vitu vingi na ndio sababu hakuna migogoro na wanyama Kijiji cha Makao kwani tunajua faida yao”alisema Mwenyekiti huyo ambaye pia ndiye diwani wa eneo hilo.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Makao John Saganda alipongeza mradi huo ikiwepo kununua vifaa kama masufuria, sahani, vijiko na vifaa vingine ambavyo vimegharimu shilingi milioni 3.7.
“Tunaahidi sisi kama walimu kutumia vizuri miradi hii ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi na lakini kuhakikisha wanapata lishe bora kwa ajili ya Afya zao”alisema
Saganda alisema pia wao kama Jamii inayozunguka maeneo ambayo Kampuni ya Mwiba inaendesha shughuli za Utalii na uhifadhi watakuwa mabalozi wazuri kuhakikisha wanyama wanalindwa na mazingira hayaharibiwi .