Na. Edmund Salaho/ Kilimanjaro.
Rais mstaafu Jakaya Kikwete leo ameongoza timu ya watu 61 kupanda Mlima Kilimanjaro ili kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasaidia watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi.
Kampeni hiyo ya kupanda Mlima Kilimanjaro ambao ni Mlima mrefu kuliko yote Barani Afrika inafahamika kama GGM KILI CHALLENGE ni mahususi kwa ajili ya kuchangisha fedha za kusaidia wenye Virusi vya Ukimwi hufanyika kila mwaka ikiwa ni ushirikiano baina ya Geita Gold Mine Tanzania na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI(TACAIDS) ambapo Mgodi wa Dhahabu wa Geita umeratibu wapandaji 61 ambapo 36 ni wapandaji Mlima kwa miguu na 25 ni wapandaji Mlima kwa Baiskeli.
Akizungumza kwenye hafla ya kuwatakia heri wapandaji wanaoanza zoezi la kupanda Mlima Kilimanjaro kwa muda wa siku saba, Mgeni Rasmi,Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ametoa ujumbe maalumu kuhusu vita ya UKIMWI na Virusi vya UKIMWI akisema.
“Kama ilivyo msemo wa sasa hivi Kazi Iendelee hivyo mapambano dhidi ya UKIMWI bado yanaendelea”
Pia Dkt. Kikwete alibainisha kuwa programu hii ya GGM Kili Challenge inachangia kukuza Utalii wa Mlima Kilimanjaro na kupongeza Watanzania na Wageni walioshiriki kampeni hiyo
“Mmefanya maamuzi sahihi na ya kishujaa Hongereni sana nitoe wito kwa watanzania kujitokeza kupanda Mlima wetu Kilimanjaro Mlima huu Mrefu zaidi Barani Afrika” alisema Dkt. Kikwete.
Aidha, Mhe.Kikwete alitoa ujumbe wa mapambano dhidi ya UKIMWI na kubainisha vita hii dhidi ya ugojwa huu inaweza kufanikiwa ikiwa kila mmoja wetu atakuwa na ushirikiano katika kutafuta ushindi.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu alibainisha kuwa Mkoa wa Kilimanjaro kwa kushirikiana na wadau wengine umekuwa ukishiriki GGM Kili Challenge katika kupambana na vita dhidi ya ugojwa wa UKIMWI ambapo kwa mwaka huu Mkoa umeweza kuchangia Kampeni hiyo Kiasi cha fedha za kitanzania Shillingi Millioni 52 ili kuunga mkono kampeni hiyo.
Mwaka huu wapandaji Mlima Kilimanjaro kupitia Kampeni ya GGM Kili Challenge wanatoka katika mataifa ya Tanzania, Afrika ya Kusini,Mpaka sasa Kampeni ya GGM Kili Challenge imechangisha jumla ya Bilioni 2.3 fedha za Kitanzania kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI.