Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Ndaki ya Kilimo, Idara ya Lishe na Sayansi ya Mlaji imefanya Mafunzo kwa Vitendo katika fani za Cultural Aspect of Clothing pamoja na Costume Designing and Construction wanaamini wataweza kutoa Mbunifu wa Vazi la Taifa au wazo litakalotoka Chuoni hapo kupitia wanafunzi wao na kutumiwa na wabunifu wakubwa nchini katika kutengeneza vazi hilo litakalomtambulisha Mtanzania.
Amebainisha hayo Bi.Zahra Majiri Mhadhiri kutoka SUA kwenye Idara ya Lishe na Sayansi ya Mlaji wakati wa Maonesho ya Bunifu za Mavazi ya aina mbalimbali ikiwemo Vazi la Taifa, Makabila mbalimbali nchini Tanzania pamoja na Mavazi ya kuvaa katika shughuli mbalimbali yaliyofanywa na wanafunzi wa Mwaka wa pili na wa tatu wa kozi ya Lishe na Sayansi ya Mlaji pamoja na Kaya chuoni hapo Julai 10, 2023 katika Kampasi ya Edward Moringe Sokoine mjini Morogoro.
Amesema katika miaka takribani mitano wanafunzi wao wamekuwa wakibuni na kuonesha mavazi ya kiasili ya Tanzania lakini pia nje ya Tanzania na mwaka huu 2023 wameweza kubuni Vazi la Taifa ambapo muelekeo umekuwa mzuri hivyo wanaimani wanafunzi hao wakiweza kupewa Maarifa zaidi kutokana na Ujuzi wanaoupata chuoni hapo, wakichanganya na wanaoupata kwenye maeneo mengine uhakika wa Vazi la Taifa kutoka SUA ni mkubwa.
“Hii ni sehemu ya somo sio kama walivyozoea kuita Fashion Show na somo hilo linaitwa Caltural Aspect of Clothing, somo lingine ni Costume designing and construction na masomo hayo yote asilimia 80 ni kwa vitendo na 20 inabaki kwenye nadharia hivyo wanafunzi wetu huwa wanapewa madhari mbalimbali zinazohusiana na ambazo zimefundishwa darasani na baadae kubuni mavazi kulingana na mandhari walizopewa”, amesema Bi.Zahra Majiri
Kwa upande wake Bw. Valentino Esau Mwinuka Mtaalam wa Nguo na Mavazi na Mhadhiri Msaidizi SUA ambaye alikuwa mmoja wa majaji katika maonesho hayo amesema mahali ambapo SUA imefikia kuna uwezekano mkubwa Mbunifu wa Vazi la Taifa kutokea chuoni hapo kwa sababu kupitia maonesho hayo ya bunifu imeonesha kabisa kuna mwanga wa kupata mbunifu huyo vilevile wapi wanaelekea katika suala zima la bunifu za mavazi.
Amesema Vijana wamejitahidi kubuni Mavazi katika maeneo mbalimbali ambayo walitakiwa kuyafanyia kazi hivyo wanatarajia kuwa kwa kadri wanavyoendelea kwa kuwa jambo hilo hufanyika kila mwaka watakaokuja Mwaka ujao 2024 wanaamini watafanya vizuri zaidi kwa sababu wameona mapungufu na mafanikio yaliyopo kwa wenzao ambao wamewatangulia.
Nao baadhi ya wanafunzi walioshirika katika maonesho hayo Hasani Mbilla pamoja na Cynthia Masuka wanafunzi wa mwaka wa tatu kutoka Kozi ya Lishe na Sayansi ya Mlaji pamoja na Kaya SUA wamesema katika maonesho hayo wamejaribu kuonesha ni kitu gani ambacho wanakifanya zaidi ili kuwajengea uaminifu na urahisi wa kufanya kazi wakati wa kuelekea Sokoni kwa ajili ya kutangaza bidhaa zao na lengo kubwa kutoa mtazamo wa Bunifu kama anasa kwenda kwenye sehemu ya Taaluma.
Wameongeza kwa kukiomba Chuo kuendelea na kile wanachokifanya cha kutoa mafunzo kwa vitendo kwa kuwa kinawafanya wanapotoka nje baada ya kumaliza masomo yao kuwa Imara kwa kujua kitu gani kinahitajika kwenye Soko hivyo wao pamoja na Chuo wanaweza kutangaza vitu ambavyo wanavifanya kwa watu wengine ili kuweza kufika mbali vilevile kuweza kujiajiri, kuajirika na kuwa chanzo cha ajira kwa wengine.