NA MWAMVUA MWINYI, PWANI
“Nimetumia kuni kwa miaka takriban kumi na mkaa nimeutumia kwa zaidi ya miaka mitano ,pamoja na mabaki ya mbao katika biashara yangu ya kuuza chips,mishkaki na kukaanga kuku”
Katika miaka yote hiyo sikujua kama nazalisha hatari katika afya yangu ,hadi pale nilipoanza kuumwa taratibu kikohozi na kubanwa mbavu wakati nikipumua “,Nakumbuka ilikuwa mwaka 2021 “anasimulia Saidi Roja almaarufu Side mkaanga chips barabarani kuelekea Mloganzila Kisarawe Mkoani Pwani.
Nilikunywa sana maziwa ,kila siku ,maana sisi wapika chips ,samaki, mama lishe ndio tunavyoshauriana kuwa maziwa ndio tiba ya kupoza moto kama unapikia mkaa mwingi ,lakini sikupona”
Side anasema ,alihangaika sana kununua dawa pharmacy, vichupa vya dawa za maji za kutuliza kikohozi,vidonge antibiotics Lakini ikawa bado anataabika,huku wengine wakimshauri atumie karafuu na mitishamba akihisi anaumwa pumu.
“Kumbe haikuwa hivyo,nakumbuka siku moja alikuja mteja wangu mkubwa kununua chips akaniona navyoendelea kuteseka na kifua, nikamuelezea ndipo aliponishauri niende hospital nikaenda Tumbi hospital pale Kibaha”
“Huwezi amini kama ndio alikuwa mkombozi wangu,!! maana ndio ikawa tiba ya ugonjwa wangu , daktari aliuliza maswali nachosumbuliwa , kama natumia kilevi,sigara!?nafanya shughuli zipi, basi nikafanyiwa vipimo na kupata matibabu ya kifua na kushauriwa nipunguze au niache matumizi ya Nishati chafu kwakuwa matumizi ya muda mrefu ya kuni na mkaa inaweza ikawa sababu ya mateso niliyoyapata”;’anaeleza Side.
Anaeleza, tangu mwaka 2021 baada ya kupata Suluhu ya ugonjwa wake alijidunduliza fedha na kuamua kununua gas ambayo anatumia kukaanga chips ,kuku licha ya kwamba mkaa kidogo anatumia kwa ajili ya kuchomea kuku na mshkaki kwa wale wanaohitaji kuchomewa.
“Nashukuru kwa kweli matumizi ya gas yananirahisishia kupika kwa haraka , gharama si kubwa kwani awali kuni na mkaa nilikuwa natumia gunia mbili kwa mwezi ambapo kila gunia 70,000 -90,000 wakati gas inachelewa kuisha na gharama ya kununua mtungi wa kg 15 ni sh.92,000 ” anaeleza Side.
Anafafanua gas inasaidia maana hata akienda mteja wa haraka anamhudumia kwa muda mfupi tofauti na mkaa au Kuni.
Nae muuza samaki ,Mama Ally mkazi wa Kibamba,anasema ana mwaka wa 25 tangu aanze kufanya biashara ya kuuza samaki kwani ndio inasaidia familia yake na watoto.
Anasema ,kwa kipindi chote hicho yeye anatumia Kuni kukaangia samaki hadi leo.
“Biashara hii nimeifanya kwa miaka mingi toka nikiwa kijana mdogo hadi sasa naelekea miaka 50 Lakini nashukuru sijapata madhara ya kiafya kwakuwa nakula chakula vizuri,maji mengi ili kupambana na moto”
“Huwa nafuata samaki feri Dar es Salaam na mzazi mwenzangu yupo kule anajishughulisha na biashara hii hii, yeye amekuwa akinishauri niachane na kuni kwakuwa wao wameshaanza kutumia gas na wanaona manufaa yake hasa katika kurahisisha muda,wanatumia muda mfupi kukaanga samaki kwa idadi wanayoitaka “anafafanua mama Ally.
Anaongeza kwamba ,tatizo kubwa linalosababisha wauza samaki ,chips wasitumie majiko ya Nishati mbadala ni kuogopa kulipukiwa na gas kwakuwa hawana elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya gas kwenye biashara hasa hizi za samaki na chips.
“Hivi mtungi wa gas nikiweka eneo la wazi hizi ,Tena tunarundikana wafanyabiashara wengi ,na huu upepo jamani si tutalipukiwa !!! naogopa sana ,labda tupate elimu juu ya matumizi yake,maana majumbani haina shida sana tunatumia ila katika biashara inaleta ukakasi” anahoji mama Ally.
Mfanyabiashara mwingine alijitambulisha kwa jina la Kulwa John, anasema wanaogopa kutumia gas kutokana na mazingira wanayofanya biashara zao , kwani wapo barabarani na wanafanya biashara zao karibu karibu hivyo wanaogopa kulipukiwa na gesi.
Unajua wale wanaofanya biashara hii kwenye vibanda vyao ni rahisi kutumia gesi ,sisi wa barabarani tunahofia maisha yetu, kwakuwa kuna hatari kubwa kutokana na umbali tuanaokaa ,unakuta mimi ninatumia gesi wa pili yangu hapo yeye anatumia mkaa, joto likizidi au cheche ya moto ikiruka tuogopa kulipukiwa “anasema Kulwa.
WATAALAMU WA AFYA
Mtaalamu wa magonjwa ya upumuaji na mfumo wa hewa ambae pia ni Mratibu wa ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB), Mkoani Pwani ,Dkt Aden Mpangile anafafanua kuwa, kama ulidhani hatari za kiafya na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya upumuaji yanasababishwa na hewa pekee umekosea, nishati chafu ya kupikia ni chanzo kingine cha majanga hayo.
Anasema, fahamu kuwa kitendo cha kuwemo jikoni kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara 300 kama unapikia nishati ya kuni au mkaa sasa jiulize wale wapika chips ,wakaanga samaki na mama lishe wanaokaa wakitumia moto wa mkaa,kuni kutwa nzima, masaa 7-8 wanapata athari kiasi gani kiafya.
“Magonjwa yanayotokana na moshi yanaathiri watu wengi lakini hayapewi kipaumbele kwa sababu dalili za magonjwa huonekana baada ya mgonjwa kuathirika kwa muda mrefu “
“Unaweza usione madhara leo ila baada ya miaka unaweza kujikuta ukiugua mfumo wa upumuaji,kushindwa kupumua kwa chanzo cha leo, “anasema Mpangile.
Anasema, kuni na hatari kwa afya yako katika maeneo mengi ya Tanzania , njia kuu ya kupika ni kwa kutumia mkaa, kuni na mafuta ya taa.
Njia hizi za kupikia hutumiwa sana kutokana na kuwa nafuu kwa familia nyingi za kipato cha chini hasa maeneo ya mjini na vijijini, ni kawaida kukuta majiko ya kupikia yenye mkaa kwenye makazi.
Lakini njia hizi za kupikia huwa na madhara ya muda mfupi na mrefu ya kiafya, Kuna athari za kiafya kwa wazalishaji wa mkaa na watumiaji.
Mpangile anasema ,mkaa kimsingi ni kaboni tupu, na mkaa unaochomwa hutoa viwango vya juu vya kaboni dioksidi, kaboni monoksidi, na vichafuzi kama vile masizi, ambavyo vinaweza kuingia ndani kabisa ya mapafu, hasa katika majiko yasiyokuwa na sehemu za kutolea hewa ya kutosha.
Athari za kiafya ,kwa matumizi ya mkaa na kuni hutoa moshi ambao huleta madhara kwa binadamu kwenye Kuni na mkaa pia hutoa chembembe ndogo ambazo huweza kupenya katika njia ya hewa na kuleta athari kiafya sanjali na hewa ya Kaboni Monoksidi inayotolewa na mkaa na kuni huweza kuingia mwilini na kupenya hadi kwenye damu kisha inaanza kuondoa hewa ya oksijeni kwenye damu, na kusababisha madhara ya muda mrefu na hata kifo kama itaingia kwa wingi.
Kaboni monoksidi, oksidi za nitrojeni, oksidi za sulphate na misombo mingine tete inayotolewa wakati wa usindikaji na uchomaji wa mkaa inaweza pia kusababisha matatizo ya kupumua na hatimaye magonjwa kama vile maambukizi ya njia ya hewa (ARI), ugonjwa sugu wa mapafu (COPD), pumu.
Anaelezea kuwa, saratani ya mapafu au kwa wajawazito kujifungua watoto wenye uzito wa chini.
Vilevile anaeleza, mkaa na kuni kwa ujumla inaweza kuathiri njia ya hewa na damu lakini mtu akishapata matatizo ya njia ya hewa kutokana na matumizi ya mkaa na kuni, inakua chanzo cha matatizo mengine ya kiafya kama kifua kikuu, moyo, unakuta mgonjwa moyo umeshindwa kufanya kazi ipasavyo lakini sababu inakua ni matatizo yanatokana na shida ya mapafu ambayo imesababishwa na matumizi ya mkaa na kuni.
Mbali na athari za ndani ya mwili, matumizi ya mkaa hususani unaotokana na kuni huweza kuathiri macho kutokana na moshi na chembembe zinatolewa.
Katika maeneo mengi ya vijijini wanatumia sana kuni kupikia pamoja na mkaa, ule moshi mara nyingi husababisha macho kuathiriwa,'” na mwisho yanakua na rangi nyekundu na wakati mwingine mtu anaweza kushindwa kuona.
Anaendelea kueleza kuwa, Kaboni Monoxide, Kaboni Monoxide (CO), ni gesi isiyo na harufu na isiyo na rangi, ni gesi yenye sumu ambayo inaweza kukufanya mgonjwa sana ukiipumua.
Inaweza kutengenezwa kwa moto na vifaa vinavyochoma gesi, kuni, mafuta au makaa ya mawe, katika majiko ya kupikia yenye sehemu ndogo za kutolea hewa, mkaa unaweza kutoa viwango vya sumu vya kaboni Monoksidi (CO).
Mpangile anabainisha, kiasi cha kidogo tu cha mkaa wa kupikia kinaweza kuzalisha viwango vya sumu ya CO, ‘Kaboni monoxide ikiingia kwenye damu inaweza kuondoa oksijeni kwenye damu na ikakaa yenyewe na ikiingia kwa wingi huweza kusababisha kifo, na madhara yake ya muda mrefu .
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali watu hufa kila mwaka kutokana na sumu ya kaboni monoksidi wanapochoma ama kutumia mkaa katika maeneo yaliyofungwa kama vile nyumba zao, kwenye kambi au magari ya kubebea watu, au kwenye mahema.
Baadhi ya waathiriwa wanakufa kutokana na sumu ya Kaboni Monoksidi baada ya kuchoma mkaa kwenye hema la chumbani au kambi ili kupata joto.
NINI CHA KUFANYA !?
Jamii nyingi za kitanzania hutumia mkaa na kuni kama njia kuu ya kupikia vyakula.
Kuacha kabisa matumizi ya mkaa huenda isiwe jambo la uhalisia kwa sasa wakati maeneo mengi hasa ya Vijijini hayajafikiwa na teknolojia mbalimbali za majiko ya kisasa.
Mpangile anaelimisha kuhakikisha unapikia na mkaa katika eneo lenye hewa ya kutosha ,katika nchi nyingi zilizoendelea matumizi ya mkaa kupikia si makubwa, na hufanywa nje maeneo ambayo yana hewa ya kutosha.
Anasema lakini nchi zinazoendelea ni ngumu bado kuepuka matumizi ya mkaa, kama jiko lako lina dirisha dogo, basi wataalamu wanashauri kupikia nje, eneo la wazi, lenye hewa ya oksijeni ya kutosha.
“Usijaribu kupika na mkaa ndani ya nyumba – haijalishi unafikiri nyumba yako ina hewa ya kutosha kiasi gani, kama unaweza tumia nishati mbadala ili kulinda afya yako.
Anaelezea, kutafuta mbadala wa kuni na mkaa ,Teknolojia imeweza kusaidia mapinduzi ya matumizi ya mkaa na kuni katika maeneo mengi duniani, lakini Barani Afrika, hususani Kusini mwa Jangwa la Sahara bado kuni na mkaa ni njia nafuu kwa familia nyingi.
Njia mbadala za mkaa ni pamoja na majiko yanayotumia umeme, gesi ya petroli iliyoyeyuka (LPG), ethanoli, majiko ya gesi yenye ufanisi kwa kutumia biomass (yaani, pellets) na biogas.
Aina mbalimbali za teknolojia za kibunifu zinapatikana pia ili kuongeza ufanisi, uwezo wa kumudu, na upatikanaji wa nishati hizi mbadala.
Ingawa mtazamo wa sasa wa biashara ya mkaa na matumizi yake yaliozoeleka si mazuri kwa Tanzania .
Kwa msaada kutoka kwa Serikali, Mashirika ya kiraia, na wajasiriamali wa sekta binafsi kupitia kupitishwa kwa kiwango cha nishati ya jua na njia nyingine mbadala za mkaa kunaweza kusababisha mamilioni ya maisha kuboreshwa na maelfu ya jamii safi na zenye afya.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dokta Gunini Kamba anasema , Kuni sumu yake inakua juu zaidi kwa kuwa moshi unaotoka unakua zaidi na Carbon dioxide inayosababisha damu kushindwa kusafirishwa kwenye oksijeni na hivyo kukata pumzi.
Anabainisha muda wa matumizi ndiyo unaozalisha madhara kwa mtumiaji kwani kwa siku chache ni vigumu kuona madhara kwa kuwa moshi huwa na chembechembe tofauti ambazo zinaenda kukaa kwenye mapafu.
Anafafanua kwamba, kiwango cha athari hutofautiana kulingana na mti unaotumika kama kuni, akifafanua ipo inayosababisha muwasho mkali ambapo nayo hupelekea matatizo ya macho.
Gunini anaelezea kwamba, jiko la kuni hutoa kati ya gramu 10 hadi 180 za monoksidi kaboni kwa kila kilo ya kuni inayotumika.
“Tunapata shida kama vile kupungua kwa viwango vya oksijeni, vinavyoathiri moyo, ikiwa viwango vinakua juu, tunaweza kupoteza fahamu na kuwa na uharibifu wa ubongo unaosababisha kifo.
Gunini anaeleza, wakati wa mwako wa kuni, dioksidi ya sulfuri hutolewa ambayo, katika mkusanyiko mkubwa, hutoa kikohozi, msongamano wa kifua, kupungua kwa kazi ya mapafu, hata bronchitis, Chembe hizi zinazosababishwa na hewa zinaweza kusababisha homa ya mapafu na pumu.
TUREJEE TAKWIMU ZA WHO
Kulingana na utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO), moshi unaotokana na kuni za kupikia ni mojawapo ya visababishi vikuu vya vifo.
Kwa mujibu wa WHO ,karibu watu milioni nne kote ulimwenguni hufa kabla ya wakati kila mwaka, kutokana na kupikia kwa moto na nishati ngumu kama mkaa.
Watafiti wanaongeza kuwa huenda athari ikawa kubwa zaidi kutokana na kutokuwa na takwimu za kutosha katika nchi hizi za Kusini mwa Janga la Sahara.
Hata hivyo, athari hii pia hugusa watoto wachanga duniani, vikigharimu maisha ya watoto 500,000 chini ya miaka mitano kila mwaka.
Utafiti huo unachambua matumizi ya nishati hizo na kuenea kwa magonjwa ya kupumua kwa watoto hao kupitia tafiti 41 zilizofanywa kwenye nchi 30 zinazoendelea kutoka bara la Asia, Afrika na Amerika ya Kusini.
Matokeo yalipendekeza jamii kuweka nje majiko yanayotumia nishati hizo ambapo tafiti zinaonyesha takriban watu bilioni tatu katika nchi zinazoendelea wanategemea kuni au mkaa kwa ajili ya kupikia.
MAONI YA WADAU KUTOKA LPG
Angella Bhoke kutoka Taifa Gas anasema endapo Taifa likipunguza matumizi ya mkaa na kuni kuna uwezekano mkubwa wa kuondoa au kupunguza changamoto ya ukataji wa miti kwani hekari zaidi ya 400,000 ya miti hupotea kila mwaka, kutokana na tatizo la ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa.
Alieleza moja ya mikakati yao ni kujenga kiwanda cha kutengeneza mitungi ya gesi kata ya Misugusugu, Mkoani Pwani ili kupunguza gharama kubwa inayotumika kuagiza mitungi ya gas nje ya nchi.
Bhoke alieleza ,hatua hiyo ni kushirikiana na Serikali katika kudhibiti uharibifu wa Mazingira na kuhimiza matumizi ya Nishati mbadala.
“Niwashauri wajasiriamali wanaotumia mkaa na kuni kama mama lishe,wauza Samaki na wakaanga chips ,kuanza kutumia Nishati safi ya gesi katika shughuli zao ili kuokoa muda na gharama kubwa wanayoitumia”
“Sisi tunaendelea kutoa elimu ,Mkoa utusaidie kupitia Halmashauri zote kutoa elimu kwa wajasiriamali na wananchi juu ya matumizi ya Nishati safi na kuwa ni rahisi kutumia, gharama nafuu na inaokoa fedha zaidi ya matumizi ya mkaa na kuni ili tuokoe miti yetu”alisisitiza Bhoke.
Jersey Ole kutoka Taifa Gas anasema kuhusu elimu ya matumizi ya gesi wanatambua umuhimu huo na wameanza kampeni ya kuhamasisha matumizi ya Nishati safi na kutoa elimu ya kujilinda .
Anaeleza , matumizi ya gesi kwa wajasiriamali na wanaotumia majumbani, yanahitaji uangalifu kwani inatakiwa kuweka gesi lako umbali wa mita 8 kutoka jiko la mkaa ili kujiepusha na madhara ya kulipukiwa na gesi.
Alikemea wale ambao huwa wakirusha mitungi wakati wa kuweka au kupanga mitungi ya gesi ,kwani ni hatari.
“Ni hatari kurusha mitungi,na hata wale wanaoagiza mitungi ya gesi kupitia madereva bodaboda jiepusheni kutumia mara tu inapofika nyumbani ni Lazima mkae japo dakika 20-30 ndio uwashe gesi lako “anasema Ole.
Ole anasema mitungi yote ni mizuri na makampuni yote yanatengeneza mitungi bora ya Nishati safi ila Taifa Gas ina mitungi bora zaidi na salama na ni mwekezaji mkubwa nchini ambae ameeneza huduma ya upatikanaji wa mitungi ya gesi na Nishati safi nchi nzima .
Anataja gharama za kununua gesi ni rahisi kwa mtungi wa kg 3.5 kiasi cha sh.29,000 ,kg 6 sh.43,000, kg 15 sh.92,000 na kg 38 sh 100,000 Bei ambazo wajasiriamali wa kitanzania wanaweza kuzimudu.
MIKAKATI YA MKOA WA PWANI
Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa ambayo inakabiliwa na athari mbalimbali zinazotokana na matumizi ya nishati chafu na uharibifu mkubwa wa Mazingira.
Kutokana na hilo juhudi kubwa zinafanyika kupitia Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,alhaj Abubakari Kunenge, kudhibiti uharibifu wa Mazingira na matumizi ya Nishati mbadala.
Moja ya juhudi zake ni kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Taifa gesi ambao wamejikita Mkoani Pwani kutoa elimu ya matumizi ya Nishati mbadala na matumizi sahihi ya gesi .
“Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kupunguza athari za moshi unaotokana na matumizi ya nishati zisizo salama kwa kuboresha upatikanaji na uhamasishaji wa wananchi kupikia nishati mbadala ambayo ni salama ili kulinda afya zao.”
“Tunataka tuwasaidie wananchi wapikie nishati mbadala ambayo ni salama kwa matumizi ili waweze kuboresha maisha yao na afya zao”
Kunenge anasema ,kwa mwaka huu mkoa umeshapanda miti milioni Tisa sawa na asilimia 82 ,lengo likiwa kupanda miti zaidi ya milioni 13.
“Mkoa huu upo karibu na Jiji la Dar es salaam,na asilimia 70 wanatumia nishati ya misitu,ambapo vijana wengi wamejiajiri katika uuzaji wa mkaa na kusababisha athari za mazingira.”
Mkuu huyo wa mkoa anasema ,kwasasa wanakuja na mkakati wa kupunguza utoaji wa vibali vya mkaa kwa asilimia 50 ili kudhibiti ukataji miti unaofanyika kwa kasi.
MIKAKATI YA SERIKALI KUU,WIZARA
Waziri wa Nishati, January Makamba, anaeleza Serikali itahakikisha inaongeza kasi ya matumizi ya gesi ya kupikia (LPG) kwa lengo la kupunguza athari za mazingira na afya za watumiaji wa mkaa na kuni hususani wajasiriamali wanaotumia mkaa na kuni.
Ameeleza kuwa kwa Tanzania asilimia 72 ya nishati inayozalishwa inatumika viwandani na asilimia ndogo sana inatumika majumbani na hiyo inayotumika nyumbani inatumika zaidi katika kuwasha taa, kupooza vitu, kupiga pasi na kiasi kidogo sana kwenye kupikia.
Ameeleza kuwa asilimia 85 ya watanzania wanapikia nishati ya mkaa, kuni, mabaki ya mazao na vinyesi vya wanyama jambo ambalo linahatarisha afya zao kutokana na moshi ambao ni sumu unaotokana na nishati hiyo .
Kutokana na hilo, Makamba anasema mpango wa Serikali ni kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia mpaka ifikapo mwaka 2033.
Takwimu zinaonesha kuwa, asilimia nane tu ya Watanzania ndio wanaotumia nishati safi hivyo Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo ndani ya miaka 10 asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi ya kupikia.
“Rais Samia ametuelekeza tutengeneze dira, mikakati na mwelekeo na pia kuanzisha mfuko wa nishati safi ya kupikia ili kuweka ruzuku itakayowawezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu bei ya gesi, hii ni kazi kubwa lakini inawezekana na kazi inaendelea,” anasema Makamba.
“Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kulivalia njuga suala la nishati safi ya kupikia ikiwa ni moja ya jitihada zake za kuboresha maisha ya Watanzania hasa kinamama.
Hata hivyo ameeleza, Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 30 kwa ajili ya kusambaza, kununua vifaa vya nishati mbadala ambavyo itavisambaza nchi nzima ili kutimiza azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama kuni kichwani.
Anawataka wajasiriamali,mama lishe na vijana kuuvaa uhusika kamili katika mazingira, kutumia Nishati mbadala ili kuongeza tija kwenye uzalishaji wa shughuli zao.
Hivi Karibuni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, alhaj dkt.Seleman Jafo alipokuwa shule ya wasichana Ruvu Sekondari Kibaha Vijijini, alieleza mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa ambayo inakabiliwa na athari za uharibifu wa Mazingira ,hivyo Jamii iongeze nguvu kutunza na kulinda Mazingira.
Jafo anahimiza wananchi kuungana kujiepusha na shughuli zinazosababisha uharibifu wa Mazingira na kupelekea mabadiliko ya tabia nchi na athari za kiuchumi .
Anasema ,lengo kubwa ni kusonga mbele katika kudhibiti uharibifu wa Mazingira, ukataji miti ili kujielekeza katika matumizi ya Nishati mbadala na safi kwa afya.