Na Mwandishi Maalum – NEC
Wapiga Kura 74,642 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 13 za
Tanzania Bara kesho Julai 13,2023.
Jumla ya
wapiga kura 74,642 walioandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huu mdogo na jumla ya vituo 205 vya
kupigia kura vitatumika.
Hayo
yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa Jacobs
Mwambegele katika Risala ya Uchaguzi huo mdogo unaofanyika kujaza nafasi wazi
za udiwani.
Jaji wa
Rufaa Mwambelegele amewataka wasimamizi
wa uchaguzi, vyama vya siasa na wagombea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu
za uchaguzi wakati wa Uchaguzi Mdogo wa madiwani katika Kata 13 za Tanzania
Bara.
Uchaguzi
huo mdogo utashirikisha, Kata ya Ngoywa katika
Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Kata ya Kalola katika Halmashauri ya
Wilaya ya Uyui mkoani Tabora na za Sindeni katika Halmashauri ya Wilaya ya
Handeni, Potwe katika Halmashauri ya
Wilaya ya Muheza, Kwashemshi katika
Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Bosha katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga zote za Mkoa wa Tanga.
Kata
nyingine ni Mahege katika Halmashauri ya
Wilaya ya Kibiti mkoa wa Pwani, Kata ya Bunamhala katika Halmashauri ya Mji wa
Bariadi, mkoa wa Simiyu, Kata ya Njoro na Kalemawe zilizopo katika Halmashauri
ya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kata ya Kinyika katika Halmashauri ya
Wilaya ya Makete mkoa wa Njombe , Kata
ya Magubike katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro na Kata ya
Mbede katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoa wa Katavi.
Aidha,
amevitaka vyama vya siasa, wagombea na wadau wa uchaguzi kuepuka kujihusisha na
matukio yenye viashiria vya uvunjifu wa amani kwani jukumu la kulinda amani ni
la kila mmoja, hivyo wahakikishe wanalinda amani iliyopo nchini.
“Jukumu la
kulinda amani ya nchi yetu ni la kila mmoja wetu wakiwemo wananchi, vyama vya
siasa, wagombea na wadau wengine wa uchaguzi,”alisema Jaji wa Rufaa Mwambegele.
Aliongeza
kuwa Sheria na Kanuni za Uchaguzi
zimeweka mamlaka na taratibu zinazotakiwa kufuatwa iwapo kutakuwepo na
malalamiko yoyote wakati wa uchaguzi, hivyo amevitaka vyama vya siasa na
wagombea kufuata taratibu hizo ili
uchaguzi huo ufanyike kwa uhuru na haki.
Mweyekiti
huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi amewataka wapiga kura wote waliojiandikisha
katika Kata 13 za Tanzania Bara kujitokeza kupiga kura ili waweze kuwachagua
madiwani wanaowataka.
Amevitaka
vyama vya siasa wagombea na wafuasi wao kuzingatia kuwa kampeni za uchaguzi
zinakamilika leo Julai 12,2023 saa 12:00 jioni hivyo hawaruhusiwi kufanya
mikutano ya kampeni kuanzia muda huo na hawaruhusiwi kutumia alama za vyama
zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi, bendera na mavazi.
Aidha Jaji Rufaa Mwambegele amevikumbusha
vyama vya Siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi huo, kuzingatia wajibu wao wa
kuweka mawakala katika vituo vyote vya kupigia, kuhesabu na kujumlishia kura.
“Upigaji
kura utafanyika katika vituo vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2020. Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa
saa 10:00 jioni. Iwapo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao walifika
kabla ya saa 10:00 jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura, mtu
yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa 10:00
jioni”alisema Jaji Rufaa Mwambegele.
Aliongeza “Tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha
62(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura 292, imeruhusu wapiga
kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho
mbadala”.
Amevitaja
vitambulisho mbadala kuwa ni Passi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au
Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
(NIDA).
Mpiga kura
aliyepoteza kadi au kadi yake kuharibika ataruhusiwa kutumia kitambulisho
mbadala iwapo tu atakuwa ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
na jina lake lipo kwenye orodha ya wapiga kura kwenye kituo anachopigia kura.
Mwambegele
amekumbusha kuwa katika vituo vya kupigia kura kipaumbele kitatolewa kwa
wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha
watakaokuwa na watoto vituoni na kutakuwa na majalada ya nukta nundu katika
vituo vya kupigia kura kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa kuona ili weweze
kupiga kura wenyewe. Alifafanua kuwa kwa wapiga kura wenye ulemavu wa kuona
ambao hawawezi kutumia majalada hayo wanaruhusiwa kwenda vituoni na watu
watakaowachagua wenyewe kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura.
Jumla ya
vyama vya siasa 17 vimesimamisha wagombea katika uchaguzi huo mdogo ambapo Tume
imevipongeza vyama hivyo na wagombea wao kwa kutumia haki yao ya msingi ya
kikatiba kujitokeza kushiriki katika uchaguzi huo mdogo wa Udiwani.
WAPIGA KURA 74,642 KUPIGA KURA KUCHAGUA MADIWANI KESHO
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele
********