Waziri wa Nishati, January Makamba amesema ujenzi mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), umefikia asilimia 90 huku akibainisha kuwa kumekuwa na mwenendo mzuri wa mtiririko wa maji yanayoingia katika bwawa hilo.
Waziri Makamba ametoa kauli hiyo jana wakati akiwa katika ziara ya kuwatembeza viongozi wa dini kutoka Baraza la Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki (TEC).
alisema hadi sasa mita za ujazo katika bwawa hilo zimefikia 163.7 za usawa bahari kutoka mita 163.61 alizozitangaza wiki iliyopita Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya mradi huo.
” Maana yake leo tungekuwa tumefunga mitambo ya kuzalisha umeme tungeanza shughuli hii.Lakini mmeona kazi ya kufunga mitambo ya kufua umeme inaendelea pamoja na nyumba ya mitambo hii shughuli yake imefikia asilimia 70,” alisema.
Alisema matarajio yao kuona Februari mwakani wakianza majaribio ya kuzungusha mitambo hiyo, kabla ya Juni mwaka 2024 kuanza rasmi shughuli za kuzalisha umeme wa megawati 2,115 utakaoingizwa katika gridi ya Taifa.
Katika hatua nyingine Waziri Makamba aliwashukuru viongozi hao wa dini wakiongozwa na askofu Lazarus Msimbe anayewakilisha Tec na askofu Mndolwa wa CCT ambaye pia ni askofu wa Anglikana Dayosisi ya Tanga.
Waziri Makamba alisema “tunashukuru Mungu ujio wa viongozi hawa wa dini waliouombea mradi na mheshimiwa Rais wetu (Samia Suluhu Hassan). Mradi huu ukikamilika utakuwa manufaa makubwa kwa Watanzania.
“Mradi wa JNHPP ukikamilika Watanzania hawatasikia kelele za mradi wa Kinyerezi umesimama kwa hiyo tutakuwa na mgao, haitakuwa hivyo kwa sababu tutakuwa na umeme wa kutosha. labda kutoka changamoto zingine za miundombinu,” alisema.
Walichokisema viongozi wa dini
Askofu Dk Maimbo Mndolwa alisema baada ya kutembea maeneo mbalimbali ya mradi huo ujumbe walioubeba ni kuwahamasisha waumini kuhifadhi na mazingira ili kuwezesha maji yanayotoka katika vyanzo mbalimbali kwenda mto Rufiji.
Alisema baada ya kutembelea wanarudi kutoka kwenye mradi huo wakiwa na moyo na ari mpya ya kuhamasisha wananchi wananchi kutunza na kuyahifadhi mazingira.
Mwakilishi wa TEC, Askofu Msimbe aliishukuru Serikali kutoa wazo la viongozi wa dini kutembelea mradi huo mkubwa wa kitaifa, akisema wametambua thamani ya viongozi katika shughuli za maendeleo ya nchi.
Alisema wanaamini mradi huo ukikamilika na kuanza uzalishaji wa nishati hiyo utakuwa mwarobaini wa kukatika umeme kunakojitokeza mara kwa mara.
“Maelezo tulioyatapata kutoka kwa watalaamu, tunadhani tatizo la kukatika umeme litakwisha, kwasababu wametueleza tutapata umeme wa kutosha na mwingine wa zaida,” alisema
“Tuna nyaraka kutoka kwa Baba Mtakatifu juu ya utunzaji wa mazingira.Tulivyotembea na kuona namna mazingira yalivyoheshimiwa wananchi watambue kuna umuhimu mkubwa wa wananchi kuendelea kutunza na kuyahifadhi,” alisema.
“Kutunza mazingira ni suala ambalo Kanisa Katoliki tunalipa kipaumbele kikubwa…Tutawaambia wamumini wetu kuendelea kuuombea mradi huu ukamilike kwa wakati, ” alisema Askofu Msimbe