Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro akipata maelezo kutoka kwa Fredrick Kalinga Kaimu Meneja wa Mawasiiano na Masoko wakati alipotembelea katika banda la TBA kwenye maonesho ya 47 ya Niashara ya Kimataifa yanayofanyika kwenye viwanja vya Sabasaba Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro akimuonesha kitu kwenye simu yake Fredrick Kalinga Kaimu Meneja wa Mawasiiano na Masoko wakati alipotembelea katika banda la TBA kwenye maonesho ya 47 ya Niashara ya Kimataifa yanayofanyika kwenye viwanja vya Sabasaba Barabara ya Kilwa jijini
Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro akizungumza na vyombo vya habari wakati alipotembelea katika banda la TBA kwenye maonesho ya 47 ya Niashara ya Kimataifa yanayofanyika kwenye viwanja vya Sabasaba Barabara ya Kilwa jijini, kushoto ni Fredrick Kalinga Kaimu Meneja wa Mawasiiano na Masoko.
Wananchi mbalimbali wakitembelea katika banda hilo
Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa TBA mara baada ya kutembela banda hilo.
…………………………………..
Na mwandishi Wetu
Serikali imesema kuwa itahakikisha miradi mbalimbali ya ujenzi wa majengo na nyumba mbalimbali za makazi na biashara kupitia Wakala wa Majengo nchini (TBA) inakamilika kwa wakati na hivyo kupunguza changamoto za ukosefu wa makazi hususani kwa watumishi wa umma, na wafanyabiashara
Hayo yameelezwa July 11, 2023 na Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro wakati akizungumza katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam ambapo amebainisha kuwa bajeti ya serikali ya mwaka 2023/2024 imeelekeza kuhakikisha ujenzi na uendelezaji wa miradi unakamilika kwa wakati.
“Tuna miradi mingi ambayo sasa hivi iko katika hatua za utekelezaji na kama mnavyofahamu wakala wa majengo Tanzania ni moja ya taasisi zilizoko chini ya wizara ya ujenzi na uchukuzi kwahiyo tuna miradi mingi ambayo tutaanza kuitekeleza mara tu fedha zitakapoanza kutoka kutokana na bajeti iliyopitishwa.” Ameeleza Arch. Kondoro.
Amesema kuwa kutokana na makusanyo ya kodi mbalimbali katika miradi iliyopo chini ya wakala pamoja na ruzuku kutoka wizarani watahakikisha ujenzi na umaliziaji wa miradi hiyo unakamilika na kwamba mwakani katika maonesho ya sabasaba watakuwa na miradi mingi ambayo watakwenda kuonesha kupitia maonesho hayo.
“Tunatarajia kuwa na ujenzi mkubwa wa nyumba Arusha pale kaloleni, na pale kutakuwa na nyumba kwaajili ya watumishi wa umma, tutatumia fedha za ruzuku kwa bajeti iliyopitishwa, lakini pia tutatumia pia fedha za makusanyo ya ndani, lakini tunafahamu kwamba kuna mradi ambao tunaendelea nao mradi wa Temeke Quarter, kuna taarifa za maendeleo ya mradi huo, tunategemea kule kujenga block saba na kila block litakuwa na nyumba mia moja arobaini na nne (144), tumeanza na block moja na tunaendelea kwahiyo fedha kadri zitakavyokuwa zinapatikana tutaendelea na mradi huo.” Ameeleza Arch. Kondoro.
Aidha Arch. Kondoro amesema, “Lakini pia pale magomeni hadi hivi sasa kuna block moja la familia 12 ambalo limekwishakamilika na watu wameashaanza kuingia na block la pili tunategemea kwamba itakapofika disemba litakuwa limekamilika, Lakini pia tunategemea kutekeleza kule kule Ghana Mwanza tumeanza ujenzi kwa kutumia vyanzo vyetu vya ndani lakini tunategemea kupata fedha za ruzuku kwaajili ya mradi huo ambao utakuwa na maduka ya biashara.”
Arch. Kondoro amefafanua kuwa katika kutekeleza agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kushirikisha sekta binafsi, kwa sasa wakala inajiandaa kuanzisha sera ya ubia ili kukaribisha sekta binafsi kuwekeza kwa njia ya ubia ikiwa ni jitihada za kuongeza ufanisi na uharaka katika upatikanaji wa mitaji, ujenzi wa miradi, kusimamia pamoja na kuongeza mapato kutokana na kuongezeka kwa shughuli za ujenzi.
“Jambo hilo tulilichukua tumelifanyia kazi ambapo maanake ilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunahuisha tamko la uanzishaji wa wakala wa majengo Tanzania, kwa maana kwamba ifikie wakati tuweze kufanya kazi na sekta binafsi, jambo ambalo tumelifanya, tumeshirika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali, Wizara, na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, sasa hivi tuko katika hatua ya mwisho kabisa ya kuhakikisha kwamba tunapata muongozo ambao utaruhusu ushirikiano na sekta binafsi.” Amefafanua Kondoro.
Wakala wa ujenzi nchini umeshiriki katika maonesho hayo na umeendelea kuwakaribisha wananchi kutembelea banda lake ili kupata taarifa na huduma mbalimbali kuhusiana na shughuli zinazofanywa na wakala hiyo, maonesho ya Kimataifa ya Biashara Maarufu sabasaba yanatarajiwa kutamatika July 13, mwaka huu.