Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angelina Mabula akimsikiliza Grace Musita Meneja Mradi wa Samia Scheme unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la taifa NHC katika eneo la Kawe jijini Dar es Salaam wakati alipokagua mradi huo leo Jumatano Julai 12,2023.
Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angelina Mabula akikaga ujenzi wa mradi wa Samia Scheme huku akiwa ameongozana na uongozi wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC.
Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angelina Mabula akizungumza na wafanyakazi katika mradi huo hawapo pichani wakati aliofanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa tatu kutoka kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Bw. Ahmad Abdalla.
Baadhi ya wafanyakazi wakimsikiliza Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angelina Mabula wakati alipokuwa akizunguma nao alipokagua mradi huo.
Majengo hayo yakiwa katika hatua mbalimbali.
Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angelina Mabula akimsikiliza Grace Musita Meneja Mradi anayesimamia ujenzi wa majengo ya Samia Scheme wakati alipokagua mradi huo katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Ahmad Abdalla.
………………………………..
NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM.
Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angelina Mabula amelitaka
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kutumia teknolojia katika utekelezaji wa majukumu ili kuongeza kasi ya ujenzi wa Nyumba katika miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini.
Akizungumza leo tarehe 12/7/2023 Jijini Dar es Salaam baada ya kukagua mradi wa Samia Scheme, Waziri Dkt. Mabula, amesema kuwa wakati umefika wa kutumia teknolojia ya ujenzi wa nyumba nyingi kwa muda mfupi na zenye ubora ili kuendana na uhitaji
Mhe. Dkt. Mabula amesema kuwa kwa mujibu wa sensa mwaka 2022 kuna uhitaji wa Nyumba 3,800,000 nchini hivyo kwa mwaka zinapaswa kujengwa nyumba 300,000.
“Naomba taasisi nyingine zinazofanya kazi ya ujenzi wa Nyumba ziongeze kasi ili kuziba pengo la ukosefu wa nyumba nchini” amesema Mhe. Dkt. Mabula.
Amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani ametoa fedha shilingi bilioni 173 kwa ajili ya kuendeleza miradi pamoja na kuanzisha miradi mipya.
Mhe. Dkt. Mabula amesisitiza kuwa hapendi kuona mradi unasimama bila sababu ya msingi kutokana na kwamba tayari fedha zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
“Naomba katika hili kila mtu awajibike, kama ni msimamizi atekeleze wajibu wake Mkurugenzi Mkuu wa NHC unaweza kumsimamisha kazi yeyote atakayezembea katika kusimamia majukumu ya shirika” amesema Mhe. Dkt. Mabula.
Amesema kuwa kila mtu kwa nafasi yake afanye kazi kwa uaminifu katika kutekeleza miradi kwa ufanisi.
Hata hivyo Mhe. Dkt. Mabula amebainisha kuwa mwaka 2024 Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji katika maonesho ya teknolojia ya ujenzi wa Nyumba, huku akitoa maagizo kwa Shirika la Nyumba Taifa kujipanga katika kufanya matangazo kwani NHC watakuwa kiongozi katika maonesho hayo.