Afisa Mwezeshaji vikundi vya hisa mradi wa Viungo Lalo Kukas akiwaelekeza wakuu wa vikundi vya hisa jinsi ya kutumia mfumo maalum (CHOMOKA) katika simu za kisasa (smartphone) wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanavikundi hao juu ya matumizi ya mfumo huo utakaowarahisishia kutunza kumbukumbu hafla iliyofanyika Ofisi za Viungo Mwanakwerekwe Zanzibar Julai 05,2023. PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR
………
Na Rahma Khamis, Maelezo 7/7/2023.
Jumla ya Vikundi 130 vya hisa katika mradi wa Viungo wanatarajiwa kupatiwa Simu aina ya Samsung Galaxy S6 ili kurahisisha kazi zao ikiwemo utunzaji wa kumbukumbu Unguja na Pemba.
Akitoa mafunzo ya kutumia mfumo maalum ujulikanao kama CHOMOKA ( PDF VSLA DIGITAL MOBILE PLAT FORM) kupitia simu za kisasa huko Ofisi za Viungo Mwanakwerekwe Afisa Mwezeshaji wa Vikundi hivyo Lalo Kukas ambae pia Mwalimu wa vikuindu vya hisa vya jamii amesema kuwa mfunzo hayo yanalenga kuwatoa wakulima katika analojia na kuwapeleka katika digitali.
Amefahamisha kuwa awali wanachama hao walikua wakitunza taarifa za hisa katika vitabu jambo ambalo lilirejesha nyuma harakati zao kwani taarifa nyingi zilipotea hivyo kupitia mfumo huo wataweza kutunza kumbukumbu kwa uhakika hususani za hisa na mikopo.
Aidha amefahamisha kuwa mfumo huo utawafanya wanavikundi hao kutumia muda mfupi katika vikao na kuweza kutumia muda mwingi katika uzalishaji.
Vile vile Kukas alisema kupitia mfumo huo kutaondoa migogoro ya taarifa tofauti za fedha kunakopelekea vikundi vingi kuvunjika.
“Tumewaletea Simu hizi kwa ajili ya kupunguza muda na kuwarahisishia kazi zenu ikiwemo usajili wa wanachama, kufanya mahesabu pamoja na kutunza kumbukumbu za kuweka na kukopa “,alifahamisha Afisa.
Afisa Kukas ameeleza kuwa katika kuhakikisha vikundi hivyo vinaondokana na matumizi ya kizamani mradi umeamua kuwawaezesha kwa kuwapatia simu aina ya Samsung Galaxy S6 bila ya malipo ambazo watatumia kwa ajili ya shuhuli zao kwa kila kikundi ambacho kipo chini ya mradi wa viungo.
Akitolea ufafanuzi juu ya mradi huo amesema mradi ni wa miaka minne na sasa wapo katika mwaka wa tatu ambapo hadi kufifikia mwisho wa mradi wanatarajia kuviifikia vikundi 200 Unguja na Pemba.
Nao washiriki wa Mafunzo hayo wamesema kupitia mradi wa viungo wanategemea mabadiliko zaidi kwani bado wanaendelea kujifunza na kuwashauri Vikundi vyengine kujiunga katika mradi huo ili kuweza kutatua changamoto zinazojitokeza katika vikunndi ikiwemo kupotea kwa vitabu.
Mafunzo hayo ya siku tano na yalishirikisha vikundi vya hisa kutoka Wilaya zote za Unguja.